Wanafunzi Watakiwa Kulinda Amani
Wanafunzi wa Shule za Sekondari katika Halmashauri ya Mji Geita wameagizwa kutoa taarifa sahihi juu ya masuala ya rushwa yanayojitokeza katika mazingira yao ili kulinda Amani iliyopo katika nchi ya Tanzania, kwani endapo watazembea na kuipoteza Amani itawawia vigumu kuitafuta pindi itakapotoweka.
Agizo hilo limetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 Ndg. Amour Hamad Amour alipokuwa akigawa zawadi kwa wanafunzi walioongoza nafasi tatu bora katika mashindano ya uandishi wa insha yaliyofanywa na klabu ya kupinga na kuzuia Rushwa katika Shule ya Sekondari Ihanamilo mjini Geita.
Ndg. Amour Hamad Amour amefafanua kuwa tatizo la rushwa limeota mizizi katika jamii yetu na linaleta athari kama wananchi kukosa huduma za afya za uhakika, vifo, kukosekana kwa ajira kwa watu wanaostahili, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kulingana na nafasi aliyonayo kuhakikisha kuwa anapambana ili kuondokana na tatizo la rushwa.
Pia amewapongeza wanafunzi watatu kutoka Shule za Sekondari Geita, Sekondari ya wasichana Nyankumbu na Shule ya Sekondari Geita Adventist kwa uhodari na ubunifu mkubwa katika uandishi wa Insha zenye mawazo ya kujenga zilizokuwa na ujumbe “ Tuungane kwa pamoja dhidi ya Rushwa kwa Amani na Usalama wa nchi yetu.”
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa amesifu jitihada za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU) Mkoa wa Geita kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha suala la vita juu ya rushwa linatekelezwa. Ameongeza kuwa, tatizo la rushwa lipo katika kila eneo ambapo shughuli za maendeleo hufanyika hivyo elimu ya kupambana nayo inatakiwa kutolewa Zaidi kwa vijana wa Taifa la leo.
“ Vijana ni lazima wajengewe mazingira mazuri kimaisha ili waweze kujikwamua kimaendeleo. Hivyo natoa wito kwa Wazazi, walimu na viongozi mbalimbali wa Serikali katika ngazi zote kuhakikisha mnawasaidia vijana hao kutimiza ndoto zao. Pia wanafunzi mnatakiwa kuwa na nidhamu kwa walimu wenu, wazazi, walezi na wanafunzi wenzenu ili kuwa na Taifa imara na lenye maendeleo.
Mradi wa klabu ya Kuzuia na kupambana na Rushwa katika Shule ya Sekondari Ihanamilo ni miongoni mwa Miradi iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2017 katika Halmashauri ya Mji Geita. Ambapo jumla ya Shilingi 1,075,000/-( Milioni moja na elfu na sabini na tano) zimetumika kufanikisha Mradi huo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa