Viongozi Wa Dini Waipongeza Serikali Mkoani Geita
Viongozi wa Madhehebu ya kikristo Wilayani Geita wametoa pongezi za dhati kwa Serikali ya awamu ya tano katika Mkoa wa Geita kwa utekelezaji imara wa miradi ya maendeleo ambayo itawanufaisha wananchi wote ndani ya Mkoa mzima.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni wakati wa ziara ya viongozi hao wakiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel walipotembelea Halmashauri ya Mji wa Geita kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ulivyofanyika na unavyoendelea.
Miradi iliyotembelewa na viongozi hao ni pamoja na Soko la wajasiriamali Katundu, Ujenzi wa Machinjio ya kisasa Mpomvu, Ujenzi wa jengo la Ofisi kuu ya Halmashauri ya Mji Geita,Hospitali ya Mkoa wa Geita, Soko kuu la Dhahabu Geita mjini pamoja na ujenzi wa jengo la Utawala kwenye eneo maalum la uwekezaji kiuchumi Magogo.
Wakiwa kwenye Mradi wa Machinjio ya kisasa Mpomvu utakaokuwa na uwezo wa kuchinja zaidi ya ng’ombe 100 kwa siku, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amewaeleza viongozi hao kuwa uwepo wa mradi huo utaibua fursa kwa wafugaji kuuza nyama na mazao ya mifugo ndani na nje ya mipaka ya nchi ya Tanzania.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, kiongozi Askofu Stephano Saguda amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa kuwa kiongozi wa kwanza aliyetambua umuhimu wa viongozi wa dini katika kuifahamu vyema miradi inayotekelezwa katika jamii yao kwa kuandaa ziara ambayo imewafumbua macho kuelewa kinachoendelea katika Wilaya yao.
Askofu Saguda aliongeza kuwa Machinjio ya kisasa Mpomvu itakapoanza kazi itawezesha upatikanaji wa ngozi ya kutosha ambayo itatayarishwa kwa viwango vya kimataifa hivyo ameishauri Serikali ya Mkoa wa Geita kuanzisha wazo la kujenga kiwanda cha kisasa cha bidhaa za ngozi halisi ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana wa Geita na kutumia raslimali hiyo ambayo haitasafirishwa kutoka mbali bali itakuwa ni ya kutoka Wilayani Geita.
Kwa upande wake Mchumi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Emmanuel Magesa amefafanua kuwa pamoja na huduma za machinjio mradi huo utahifadhi mazingira kwa kutibu maji machafu na kuwa masafi kwa matumizi ya kawaida pamoja na kuzalisha gesi itakayotumika kwa shughuli mbalimbali
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa