Familia Zakumbushwa Wajibu wa Malezi ya Watoto
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu amewataka wazazi na walezi kutambua kuwa ni jukumu la kila mmoja wao kuwalinda, kuwatunza na kuwaendeleza watoto wa Taifa hili kwa sababu watoto ni Taifa la leo ambapo msingi wa baadaye wao ndio wanaoutengeneza.
Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika Kata ya Ludete Mamlaka ya Mji mdogo Katoro hivi karibuni. Wakati wa Maadhimisho hayo Waziri pia alizindua kitini cha Ajenda ya wajibu wa wazazi wa Malezi na matunzo ya familia nchini Tanzania.
Aidha Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali imeshatoa maelekezo ya kuanzishwa kwa madawati ya ulinzi wa watoto shuleni ili kuboresha mfumo wa upatikanaji wa huduma kwa wahanga wa ukatili na kuimarisha ulinzi wa watoto wawapo shuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa wanaume katika Mkoa wa Geita waache tabia ya kuweka heshima kwenye maduka ya pombe kwa kutumia fedha nyingi kwenye ulevi. “ Heshima ya mwanaume ni kuwa na uwezo wa kutunza , kuihudumia na kuipenda familia yake hususani mke na watoto ili kuwa na familia zenye maadili yanayokubalika katika jamii.
Akisoma Risala kwa niaba ya watoto wenzake, Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Mkoa wa Geita mwanafunzi,Joseph Francis amesema watoto wa Mkoa wa Geita bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazingira hatarishi ya watoto kama kufanya kazi katika migodi pia baadhi ya wazazi huwaachisha shule watoto wao na kuwaingiza kwenye biashara ndogo ndogo ili kujipatia kipato cha familia nzima.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 kila mwaka kuwakumbusha watoto hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Soweto Afrika ya kusini katika kulinda zao ambapo watoto waliandamana kupinga aina ya elimu duni ya kibaguzi waliyopewa na Serikali ya kibeberu pia walitaka Serikali ya Mzungu iwape ruksa kufundishwa kwa lugha zao wenyewe. Kauli Mbiu ya Mwaka 2019 inasema “Mtoto ni msingi wa Taifa endelevu; tumtunze, tumlinde na kumuendeleza.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa