Kaya Hewa Kuondolewa Kwenye Mpango wa TASAF
Uhakiki wa wanufaika wa mpango wa TASAF awamu ya tatu katika Halmashauri ya Mji wa Geita ambao unaendelea utawezesha wanufaika wote ambao hawana sifa za kupokea ruzuku inayotolewa na Serikali kuondolewa katika utaratibu huo.
Akizungumza katika mafunzo kwa wawezeshaji ngazi ya Halmashauri katika Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni Mwezeshaji Mkuu kutoka makao makuu ya TASAF Bi. Graceana Maganga amesema kuwa zoezi la uhakiki wa kaya maskini ambazo zinanufaika na fedha za mfuko wa TASAF linafanyika katika Mkoa mzima wa Geita kwa lengo la kubaini kaya hewa na kuziondoa katika orodhaya malipo.
Bi. Graceana ameongeza kuwa zoezi la uhakiki litafanyika kwa njia ya kielektroniki ambapo wawezeshaji katika ngazi ya Serikali za mitaa watatumia vifaa vya kisasa kujaza taarifa za wanufaika kwa kutumia kishikwambi (Tablet) kwa kuongozwa na maswali ya dodoso ambalo limeandaliwa na TASAF.
Kwa upande wake Afisa Mradi wa TASAF kutoka Makao Makuu ndg. Mary Mtambalike amesema kuwa zoezi la uhakiki linafanyika baada ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuagiza kaya zote ambazo hazina sifa ya kuwa maskini, kaya zenye watumishi au viongozi wa Serikali, watu wenye uwezo kiasi kiuchumi na waliofariki wanaondolewa na kuwapatia fedha watu wanaostahili na wenye sifa za kuitwa maskini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa Halmashauri itashirikiana kikamilifu na TASAF kuhakikisha kuwa kaya zote ambazo hazina vigezo vya kuwa maskini au wale ambao walishaondoka kwenye kundi la maskini wanaondolewa kwenye orodha ya wanufaika.
Mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini unatoa huduma kwa kaya maskini ili kuziwezesha kujenga uwezo wa kiuchumi kwa kuwalipa fedha taslimu wanufaika ili waweze kufanya shughuli ndogo ndogo za kiuchumi ili wajikwamue kimaisha na kuzihudumia familia zao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa