Geita Mji Yang’ara kwa Utoaji Mikopo
Halmashauri ya Mji Geita imefanya vizuri kwa kutimiza agizo la Serikali la kutoa asilimia kumi(10%) ya bajeti yake kama Mikopo kwa vikundi vya vijana na kina mama wanaojishughulisha na kazi mbalimbali zinazowakwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa utoaji wa Hundi kwa vikundi sita vya vijana na wanawake wajasiriamali kutoka kata mbalimbali za Halmashauri ya Mji Geita wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kalangalala. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita, Mh. Leonard K. Bugomola amesema kuwa Halmashauri ya Mji Geita inatambua na kuthamini shughuli za kiuchumi zinazofanywa na vijana pia wanawake walio jisajili katik a vikundi, hivyo kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetenga bajeti ya Shilingi Milioni Mia tano( 500,000,000/-) zitakazokopeshwa kwa vikundi vilivyosajiliwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita.
Hundi tofauti zenye jumla ya Shilingi Milioni thelethini(30,000,000/-) zilitolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2017 Ndg. Amour Hamad Amour kwa vikundi sita vya wanawake na vijana waliojiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Halmashauri ya Mji wa Geita.
Ndg. Amour ameipongeza Halmashauri ya Mji Geita kwa kutoa fedha inayotosheleza kulingana na agizo lililotolewa na Serikali la kutenga asilimia 10% ya bajeti yake kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana waliojiajiri. Aliwataka Wakurugenzi ambao wanakwepa kutoa fedha hizo kiutaratibu waige mfano wa Halmashauri ya Mji Geita.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 alitoa pongezi kwa vijana waliojikwamua kwa kujiajiri katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kwa kuzalisha. bidhaa zenye viwango na zinazovutia. Kadhalika aliwataka wawe mabalozi wazuri kwa vijana ambao wako mitaani na hawataki kujishughulisha bali hushinda wakicheza bao na kutoa shutuma zisizofaa kwa Serikali.
Pia aliwaagiza wataalam wa Idara ya Maendeleo ya jamii kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana hao na kuwasaidia kuwatafutia vifungashio bora vya bidhaa zao ili kukidhi ushindani wa biashara kitaifa na kimataifa. Ndg. Amour aliwashauri wataalam hao kujifunza juu ya kilimo cha nyumba ya kijani (green house) kwani ni kilimo kilicho katika soko la biashara kimataifa ili wawashawishi vijana katika umoja wao kulima kilimo hiki chenye tija.
Ndg. Amour Hamad Amour alitoa wito kwa Halmashauri ya Mji Geita kuunda SACCOS itakayotumika kupewa fedha zote ambazo wanavikundi walio ndani ya SACCOS watakopeshwa fedha hizo. Hii itasaidia usalama wa fedha inayokopeshwa kuwa wa uhakika zaidi kuliko utaratibu unaotumika hivi sasa wa kukopesha vikundi moja kwa moja.
Ukiwa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mwenge wa Uhuru umezindua, kufungua, kuweka mawe ya msingi katika Miradi kumi ambapo miradi minne ilitembelewa. Miradi yote ina thamani ya Shilingi 9,177,774,739.73 ambapo Halmashauri imechangia Shilingi 259,620,989.73, Serikali kuu imechangia Shilingi 331,692,500 na Shilingi 8,586,461,250 ni nguvu kazi za wananchi.
Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 ni “SHIRIKI KUKUZA UCHUMI WA VIWANDA KWA MAENDELEO YA NCHI YETU”.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa