Shilingi Bilioni 2 Kujenga Uwanja wa Kisasa
Halmashauri ya Mji wa Geita imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo katika mtaa wa Magogo Geita mjini ambapo katika awamu ya kwanza ya ujenzi jumla ya shilingi 2,040,312,754.92 za kitanzania chanzo cha fedha ni wajibu wa kampuni kwa jamii(CSR) kutoka mgodi wa GGM zitatumika kutekeleza mradi huo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa ujenzi wa uwanja huo baina ya Halmashauri ya Mji wa Geita na mkandarasi EFQ Company Limited akishirikiana na Mugoo Construction Limited wa jijini Mwanza katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo ameipongeza Halmashauri ya Mji Geita kwa maamuzi ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo.
Mhe. Shimo amesema ana imani kuwa ushirikiano baina ya wakandarasi wawili utawezesha shughuli ya ujenzi wa uwanja kukamilika ndani ya kipindi kilichokubalika kwenye mkataba, kazi zinazowezekana kufanywa usiku na mchana zifanyike bila visingizio vya aina yoyote ili uwanja huo uweze kuwanufaisha wakazi wa Geita na kuifanya tasnia ya michezo kuitangaza Halmashauri na fursa zilizomo ndani ya Mji wa Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ametoa rai kwa wadau wa vyama vya michezo katika Wilaya ya Geita kuweka mkakati wa kuandaa timu nyingine za daraja la I ili ziendelee kuleta hamasa ya michezo katika Wilaya ya Geita. Kadhalika wahakikishe timu ya Geita Gold ambayo imepanda daraja na kuingia ligi kuu inanolewa, kutunzwa, kuboreshwa ili inapoingia ligi kuu isiwe na hofu ya kushuka daraja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhe. Costantine Morandi amewataka wakandarasi waliopata nafasi ya kujenga uwanja huo kufanya kazi haraka na kwa weledi mkubwa ili uwanja huo uweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia fursa wananchi wa Geita kutazama mechi za timu yao wakiwa nyumbani. Pia ametoa sukrani za dhati kwa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Geita (GGM) kwa ufadhili wao mkubwa katika sekta ya michezo na kuwasihi kuendeleza ushirikiano huo.
Halmashauri ya Mji wa Geita imetenga eneo lenye Hekta 10.4(104,570sqm) kwa ajili ya kujenga uwanja wa kisasa wa michezo ambao ndani yake kutakuwa na kiwanja cha mpira wa miguu, njia za mchezo wa riadha ,maeneo ya biashara na maegesho ya magari. Uwanja huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa wa kuingiza watazamaji 12,000 wote wakiwa wameketi.
Katika awamu ya kwanza ya ujenzi miundombinu muhimu itakayojengwa ni pamoja na Jukwaa kuu, kiwanja cha mpira wa miguu, vyumba vya wachezaji, chumba cha waamuzi, chumba cha kupima wachezaji,chumba cha huduma ya kwanza, Ofisi ya meneja wa uwanja na chumba cha mikutano, uzio wa ukuta wa tofali na milango ya kuingilia na uchimbaji wa kisima kirefu cha maji na matanki ya kuhifadhi maji kwa ajili ya ujenzi na matumizi ya uwanja.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa