GEITA YOUTH GROUP WAKABIDHIWA GARI
Kikundi cha vijana wa Geita Youth wamekabidhiwa rasmi lori aina ya FAW pamoja na mashine mbili za kufyatulia matofali kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita Tarehe 15/4/2020 katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Geita. Gari na mashine hizo vikiwa ni mali zilizonunuliwa kutoka kwenye fedha kiasi cha Shilingi 163,025,000/= zilizotolewa kama mkopo na Halmashauri ya Mji wa Geita mapema mwezi Machi 2020.
Akipokea gari hilo na kuzungumza kwa niaba ya wanakikundi wenzake, Mwenyekiti wa kikundi hicho Ndugu Gabriel Nyasilu ameshukuru uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kukubali andiko lao na kuwapatia kiasi kikubwa cha mkopo walioomba ili waweze kuendesha shughuli zao zitakazowakwamua kiuchumi.
Ndg. Nyasilu ameahidi kuwa wanakikundi wataenda kufanya kazi kwa bidi na weledi mkubwa kama timu na hawahitaji kuingia katika dhambi ya kukwamisha vikundi vingine vya vijana kukosa mikopo kutoka Halmashauri endapo wao watashindwa kurejesha mkopo huo kama makubaliano baina yao na Halmashauri yalivyoainishwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhe. Leonard Bugomola amewasihi vijana hao kuonyesha mfano wa kikundi bora na chenye dira kwa jamii ili vikundi vingine viige mfano kutoka kwao. Pia amewatahadharisha kutoharibu uaminifu uliojengwa kwao na Halmashauri ya Mji Geita kwa kutenda jambo lolote kinyume na makubaliano kwa sababu hali hiyo itavunja Imani ambayo jamii nzima imeijenga juu yao.
Kwa uande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Ndg. Mwinyiheri Baraza ameipongeza Halmashauri ya Mji Geita kwa kuwa Halmashauri ya Mji ya kwanza kutekeleza utoaji wa mkopo mkubwa kwa vikundi vya vijana, kadhalika amewataka vijana kuwaonyesha viongozi wa Geita Mji kuwa hawakufanya makosa kuwakopesha Milioni 163 bali mkawe chachu ya kuleta maendeleo katika jamii.
Diwani wa Kata ya Kasamwa Mhe. Mary Kasanda na Diwani wa Kata ya Kalangalala Mhe. Zephania Mahushi kwa pamoja wamewataka vijana hao kuungana, kushirikiana kikamilifu katika kutunza mali hiyo ili waweze kufanikisha malengo yao waliyojipangia na hatimaye waweze kurejesha fedha walizopatiwa na Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo zitatumika kunufaisha vikundi vingine vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vilivyo na mahitaji mbalimbali.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa