Geita Mji Yaweka Historia Mikopo ya Makundi Maalum
Halmashauri ya Mji wa Geita kwa mara ya kwanza imewezesha kikundi kimoja cha Geita Youth Group kutoka Kata ya Kalangalala mkopo wa shilingi 163,025,000/= kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa kufyatua tofali, ununuzi roli na kiasi cha fedha kwa ajili ya uendeshaji wa mradi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya mkopo huo hivi karibuni katika Ukumbi wa GEDECO Halamshauri ya Mji Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Josephat Maganga amewaasa wanakikundi hao kutobadili tabia na mienendo yao kutokana na ujio wa fedha hizi, pia hakikisheni fedha hizi mnazitumia kufanikisha mipango mliyoipanga kama kikundi .
Mkuu wa Wilaya ya Geita amesema kuwa vijana wa Geita Youth wamebuni mradi wenye faida kwa sababu matofali yanahitajika sana katika kipindi hiki ambapo kuna kampeni kubwa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwezesha watoto wote waliofikia umri wa kuanza shule hawakosi shule na wanafunzi wa sekondari wanapata madarasa ya kujifunzia.
Mhe. Josephat Maganga pia alipongeza Baraza la Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwa mfano bora na wa kuigwa katika kutelekeza maagizo ya Serikali kwa kutoa sehemu ya mapato yake kama mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Geita Youth Ndg. Manjale Magambo ametoa pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Mji Geita kwa kuwasaidia vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo inayowawezesha kutekeleza miradi mbalimbali na hatimaye kujikwamua kimaisha. Kadhalika ameahidi kuwa yeye na kikundi chake watatumia mkopo huo kama walivyopanga katika andiko lao la mradi na si kukopeshana fedha hizo mtu mmoja mmoja.
Sambamba na mkopo kwa kikundi hicho jumla ya Shilingi 200,025,000/= zimetolewa kwa vikundi 3 vya wanawake, 3 vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuendeleza miradi yao ya kiuchumi, ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya shilingi 598,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kukopesha makundi maalum. Pia Halmashauri ya Mji imetoa pikipiki mbili kwa ajili ya kuwarahisishia Maafisa Maendeleo ya Jamii usafiri wanapokwenda kwenye shughuli zao za kila siku.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa