Elimu Ya COID-19 Kujenga Uelewa Mkubwa Kwa Jamii
Mafunzo juu ya uelewa wa kina kuhusu Virusi vya COVID-19,namna inavyoambukiza na jinsi ya kujikinga yaliyotolewa na wataalam wa elimu ya Afya kwa Umma kutoka Halmashauri za Wilaya na Geita mji kwenda kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii yamebainishwa kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Wilaya ya Geita.
Hilo limebainishwa na washiriki wa mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kujilinda na maambukizi ya Virusi vya Corona yaliyofanyika Tarehe 22-23/04/2020 katika Chuo cha Uuguzi na Ukunga Geita Mjini kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka katika mitaa na Kata mbalimbali za Wilaya ya Geita, Mafunzo ambayo yamefadhiliwa na Shirika la Plan International.
Bi. Suzana Kazige Sindano ambaye ni Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka Kijiji cha Chibingo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ametoa wito kwa washiriki wenzake kutumia elimu waliyoipata kufikisha ujumbe toshelezi kwa jamii inayowazunguka ili waelewe kiundani juu ya mlipuko wa Virusi vya Corona. Pia amelishukuru Shirika la Plan kwa kuwaletea wataalam wa Afya kuwapatia elimu juu ya ugonjwa huo ulioitikisa dunia.
Kwa upande wake Ndg. Nathanael Kagoma, Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka mtaa wa Lutozo Halmashauri ya Wlaya ya Geita amesema jamii yake bado haijaelewa kiundani kuhusu namna ya kujilinda au kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID-19 . Elimu waliyoipata kutoka kwa wataalam wa afya imewapa mbinu mpya za ufundishaji utakaorahisisha jamii yake kupambana kikamilifu katika kujikinga na virusi vya COVID-19.
“Mara kwa mara nimekuwa nikisikia maelekezo ya namna ya kuepukana na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa kusikiliza matangazo yanayorushwa na kituo cha Redio ya Storm FM, lakini leo nalishukuru sana Shirika la Plan kwa kutambua umuhimu wetu na kutuwezesha kupata elimu ya ana kwa ana pia kujifunza kwa vitendo jinsi ya kunawa mikono, kuvaa barakoa,kutumia vitakasa mikono na mengineyo ambayo yatawawezesha kufikisha ujumbe halisi kuhusu Virusi vya COVID-19 kwa jamii wanayoihudumia”. Alisema Bi. Anna Kassala, Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Kata ya Kanyala Halmashauri ya Mji Geita.
Ndugu Selestine Dominick Mafunganya, Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka Mtaa wa Kaduda Wilayani Geita amedhihirisha furaha yake kwa kuwashukuru Plan International kwa kuwakutanisha wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Geita ambapo baada ya mafunzo watapata fursa ya kubadilishana mawazo juu ya mbinu watakazozitumia kufikisha elimu ya COVID-19 kwa jamii. Kadhalika ameeleza kuwa atashirikiana na uongozi wa mtaa wake kufikisha elimu katika maeneo ya masoko, makanisani, msikitini, vikao vya Kamati za Mitaa na Kata ili watu wengi waweze kunufaika na elimu juu ya mapambano ya ugonjwa wa Corona.
Shirika la Plan International limewezesha mafunzo kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii kutoka mitaa na vijiji mbalimbali ndani ya Wilaya ya Geita ikiwa ni jitihada za shirika hilo kuhakikisha linashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona ambao unaendelea kuutikisa ulimwengu mzima.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa