Ziara Za Mafunzo Kuboresha Kiwango Cha Ufaulu
Walimu kutoka katika Shule za Msingi na Sekondari ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita ambazo hazikufanya vizuri kitaaluma hususan katika mitihani ya kuhitimu mwaka 2020 na miaka ya nyuma wameshauriwa kufanya ziara za mafunzo kwenye shule ambazo zina ufaulu mzuri.
Ushauri huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mheshimiwa Joseph Lugaila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao cha wadau wa elimu waliokutana kujadili kwa pamoja maendeleo ya sekta ya elimu katika Halmashauri ya Mji wa Geita kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu hivi karibuni.
Mhe. Lugaila aliongeza kuwa ziara za mafunzo katika shule zinazofanya vizuri kitaaluma zitawawezesha walimu wa shule zinazofanya vibaya kujifunza mbinu za kufundisha na masuala mengine muhimu yatakayowawezesha kupandisha kiwango cha ufaulu katika shule zao. Pia wahakikishe wazazi na walezi wa wanafunzi wanashirikishwa katika vikao mbalimbali na mipango yote iliyopangwa kutekelezwa shuleni.
Akiongelea mikakati iliyowekwa na Idara yake ili kupandisha kiwango cha ufaulu, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Geita Mwl. Rashid Muhaya amesema kuwa wameazimia kuendesha mafunzo kazini kwa walimu ili kuwaongezea maarifa na ujuzi katika kufundisha, kuendeleza program ya kufundisha masaa ya ziada ili kukamilisha mihtasari ya masomo mapema, kufanya mitihani ya pamoja kwa wanafunzi wa kidato cha pili, nne na sita ili kuongeza ushindani wa shule na shule na kutoa tuzo na zawadi kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Kwa upande wa Idara ya Elimu msingi Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Margareth Macha amesema idara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu tumedhamiria kuondoa kabisa tatizo la wanafunzi wasiomudu kujua kusoma,kuhesabu na kuandika kwa kuwapa walimu mbinu na mafunzo mbalimbali na kufanya tathimini ya maendeleo ya KKK kila mwisho wa mwezi.
Kadhalika Idara ya Elimu msingi imedhamiria kuwahamasisha wazazi na walezi kupitia umoja wa wazazi/walezi na walimu shuleni kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa mwendelezo kuanzia nyumbani ili kuinua viwango vya taaluma. Pia idara itatembelea shule 10 duni mara kwa mara ili kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakwamisha na kuzitatua kwa pamoja.
Katika kikao hicho shule zilizofanya vizuri kitaaluma zilipewa zawadi ya vyeti na fedha taslimu sambamba na wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani ya kitaifa kama motisha ya kuwafanya wazidi kukazana na kufanya vizuri zaidi kitaaluma, kadhalika Shule ya Msingi Bung’wangoko ilipewa kinyago kwa kuwa shule ya mwisho kitaaluma .
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa