Zaidi ya Shilingi Biloni 9 kutekeleza Miradi ya Jamii
Halmashauri ya Mji wa Geita na Wilaya ya Geita zitapokea kiasi cha shilingi Bilioni 2.9 kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita( GGM) kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya kijamii kwa mwaka 2019.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya kusaini hati ya Mkataba wa Makubaliano baina ya Kampuni ya GGM na Halmashauri zote mbili katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameushukuru Mgodi wa GGM kwa kuendelea kushirikiana vyema na Serikali na kuwa kampuni ya kwanza iliyotekeleza sheria ya Serikali inayozitaka kampuni za uchimbaji madini kuandaa mpango unaotekelezeka wa uwajibikaji kwa jamii inayowazunguka.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema kuwa fedha hiyo itatumika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambayo baadhi ni ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu, ujenzi wa soko kubwa la katundu ambalo litaleta heshima kwa wajasiriamali wadogo, ujenzi wa chuo kikuu huria cha Tanzania Tawi la Geita na ujenzi wa uwanja wa mpira wa kisasa.
Mhandisi Robert Gabriel pia ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwa ya kwanza katika Halmashauri zote nchini kwa ukusanyaji wa mapato ghafi, pia ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 157 na kuifanya kuwa miongoni mwa halmashauri tano zilizopeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mheshimiwa Leonard Bugomola ameushukuru mgodi wa GGM kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa mchango wao ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita na kuiwezesha Halmashauri kuwa ya kwanza kitaifa kwa ukusanyaji mapato. Pia ameshauri maandalizi ya miradi ya CSR mwaka 2020 ianze mapema kuliko kusubiri katikati ya mwaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GGM , Richard Jordinson amesema kuwa fedha iliyopangwa katika mwaka 2019 itatumika kutekeleza miradi ya afya, mazingira, elimu, kilimo na miundombinu. Kadhalika kampuni yake inaamini kuwa kushirikiana na jamii inayowazunguka kutaonyesha uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza na kuitunza miradi ya maendeleo .
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa