Zahanati ya Nyanguku Kuokoa maisha ya Wananchi
Wananchi wapatao 11,359 ambao ni wakazi wa vijiji vya Nyanguku, Shinamwenda, Mwagimagi na mtaa wa Nyakato katika kata ya Nyanguku, Halmashauri ya Mji Geita watanufaika na huduma za afya kwa karibu baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Zahanati katika kata yao.
Akifungua rasmi Zahanati hiyo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ametoa pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Mji Geita na wananchi wa Nyanguku kwa kufanikisha upatikanaji wa Zahanati hiyo ambayo itakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa kata hiyo na vijiji vya jirani. Pia ametumia fursa hiyo kuwashauri kuitunza Zahanati hiyo na kujipanga kuanzisha ujenzi wa Shule ya Sekondari katika kata hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo Diwani wa Kata ya Nyanguku Mh. Elias Ngole amesema kuwa kwa miaka yote wananchi walikuwa wakitembea umbali wa kilometa kumi kwenda zahanati ya Bunegezi iliyoko kata jirani kwa lengo la kupata huduma za afya, hali ambayo ilikuwa ikisababisha vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga.
Mh. Ngole amewashukuru wananchi wa Kata ya Nyanguku kwa kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha wanachangia ujenzi wa Zahanati hiyo pamoja na nyumba pacha mbili kwa ajili ya watumishi wa zahanati hiyo. Pia ameshukuru uongozi wa Halmashauri ya Mji Geita kwa kuthamini afya za wakazi wa Nyanguku na kutambua uhitaji wao wa kupata zahanati katika kata yao.
Diwani wa Kata ya Nyanguku ameongeza kuwa wananchi wa Kata yake wameweka mpango mkakati wa kuongeza majengo mawili kwa ajili ya kulaza wagonjwa ili zahanati yao iweze kupandishwa hadhi ya kuwa kituo cha afya siku za mbeleni.
Ujenzi wa Zahanati ya Nyanguku ulianza mwaka 2014 ambapo jumla ya Shilingi Milioni 168,742,000/= za kitanzania ambazo ni mchango kutoka Serikali kuu, Halmashauri ya Mji Geita na Shilingi Milioni tano pamoja na nguvu kazi ikiwa ni mchango wa wananchi wa Kata ya Nyanguku.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa