Wizara ya Elimu Kuendelea Kujenga Miradi Geita Mji – Mhe. Olenasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Tate Olenasha amesema kuwa Wizara yake itaendelea kutoa fedha ya ukamilishaji wa miradi yote ya majengo ya madarasa, Ofisi na nyumba za walimu ambayo imefikia hatua ya maboma yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Mhe. Olenasha ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi kukagua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi ya mthibiti wa shule pamoja na kutembelea shule za Msingi Mbugani,Mwatulole Sekondari na Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu tarehe 01/08/2019 ambapo pia alizungumza na wanafunzi wa shule hizo.
Naibu Waziri wa Elimu ameongeza kuwa wizara itajenga madarasa mawili, chumba cha kupimia afya za watoto na nyumba moja ya walimu wa kitengo cha elimu maalum katika Shule ya Msingi Mbugani kitengo cha elimu maalum, ambapo pia amempongeza Mkurugenzi na Halmashauri ya Mji Geita kwa ujenzi wa bweni la watoto wenye ulemavu ambalo limefikia hatua inayoridhisha.
“Serikali inatambua umuhimu wa watoto wenye ulemavu mbalimbali hivyo itahakikisha inawekeza kwenye vitengo vya elimu maalum ili watoto wenye mahitaji maalum waweze kusoma vizuri na hatimaye kufikia malengo yao, nanyi watoto endeleeni kutumia fursa iliyotolewa na Serikali kuhakikisha mnafika mbali” Aliongeza William Olenasha.
Naibu Waziri wa Elimu alitoa pongezi kwa Mthibiti ubora wa shule kanda ya ziwa kwa ujenzi wa ofisi ya Mthibiti ubora wa shule Halmashauri ya Mji Geita hususan kwa kutumia utaratibu wa force akaunti unaotoa fursa kwa vijana walikoko katika eneo husika kupata ajira za ujenzi na kuagiza Halmashauri ihakikishe ujenzi huo unamalizika kwa wakati na viwango vilivyokubaila.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Bi. Mariam Mkaka akizungumza kwa niaba ya mbunge amewasilisha ombi la kukarabatiwa kwa shule kongwe za Msingi Ukombozi na Sekondari ya Geita ambazo zimechakaa sana kwa sasa. Ambapo Naibu Waziri wa Elimu ameahidi kulifaanyia kazi suala hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi( CCM) Wilaya ya Geita Ndugu Barnabas Mapande ametoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha miundombinu ya majengo ya shule kwa ujenzi wa madarasa na mabweni ya kisasa ambayo hayakuwepo kipindi cha nyuma, hivyo wanafunzi watumie nafasi hiyo kwa kusoma kwa bidii na kumuombea afya njema Rais John Pombe Magufuli na Baraza lake la Mawaziri ili waendelee kufanya kazi kwa bidi kwa maendeleo ya Taifa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa