Wafanyakazi Jengeni Mikakati ya Kutatua Changamoto Zenu- RC Geita
Mkuu wa Mkoa wa GeitaMhandisi Robert Gabriel amewashauri wafanyakazi katika Mkoa wake kujenga mshikamano katika kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku kwenye maeneo yao ya kazi ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Mkuu wa Geita ametoa rai hiyo Tarehe 01 Mei 2019 wakati wa Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Chato, wilayani Chato Mkoa wa Geita.
Mhandisi Robert Gabriel ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyakazi wote kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa, uaminifu na uadilifu na kutendea haki weledi walionao wakiongozwa na miiko ya kazi na taaluma zao.
“Kumbukeni kuwa kutoa huduma kwa wateja wetu ni wajibu wenu hivyo jiepusheni kabisa na kupokea rushwa ya aina yeyote, kwa wale wanaojihusisha na suala la rushwa waache mara moja fanyeni Geita pawe mahala patakatifu” . Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mhandisi Robert Gabriel amewatahadharisha Wafanyakazi kuendelea kujikinga na Ugonjwa wa UKIMWI kwa kuwausia kuwa waaminifu, kujizuia na kusubiri pia kila mmoja kujenga utamaduni wa kupima afya kila wakati ili kufahamu hali zao na kuchukua hatua zinazostahili kupambana na ugonjwa huo. Kadhalika kutowanyanyapaa ndugu na jamaa ambao walioambukizwa bali wawafariji, wawapende, kuwatia moyo na kushiriki pamoja nao katika shughuli za kijamii.
Akibainisha changamoto zinazowakabili Wafanyakazi wa Mkoa wa Geita, Mwenyekitiwa Shirikisho laVyama vya Wafanyakazi Ndugu Ramadhan Pangala amesema kuwa malimbikizo ya madeni, mishahara midogo, ucheleweshwaji wa kupandishwa madaraja na baadhi ya wafanyakazi wa migodini kulipwa mishahara kupitia Serikali za Mitaa na kutokuwa na maduka ya Dawa vijijini kwa ajili ya kuwahudumia wanachama wa Bima ya Afya bado ni changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa Mkoa huo.
Ndg. Pangala ametoa rai kwa Serikali kuwahamishia Hazina watumishi wote wanaolipwa mishahara kupitia mapato ya ndani kwani watumishi hao hawapati stahiki yao kwa wakati kama ilivyo kwa watumishi wengine.
Siku ya Wafanyakazi Duniani huadhimishwa Mei mosi kila mwaka kwa lengo la kukumbuka harakati na jitihada zilizofanywa na wafanyakazi wakati wa mapinduzi ya viwanda huko Ulaya. Kwa mwaka huu Madhimisho hayo yalibeba kauli Mbiu isemayo “Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, Wakati wa Mishahara na Maslahi kwa Wafanyakazi ni Sasa.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa