Wazazi Watakiwa Kuwa Sehemu ya Elimu ya Watoto
Wazazi katika Halmashauri ya Mji wa Geita wameshauriwa kubadilisha tabia na kuwa mstari wa mbele kufuatilia maendeleo ya watoto wao wanaokwenda shule, pia kujitahidi kushirikiana kikamilifu na Serikali katika kuboresha miundombinu itakayowawezesha wanafunzi kujifunza vizuri.
Ushauri huo umetolewa na wadau mbalimbali wa elimu walipokutana katika kikao cha pamoja kujadili vikwazo na vizuizi vinavyopelekea kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika Halmashauri ya Mji na mikakati ya kukabiliana na vikwazo hivyo. Kikao hicho kimefanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Ndugu Mwinyiheri Baraza amesema kuwa inasikitisha kuona mzazi hatambui umuhimu wa elimu ambayo mtoto ameifuata shule.Asilimia kubwa ya wazazi hawafahamu watoto wao wanajifunza mambo gani wawapo shule na kutofuatilia mienendo ya kitaaluma na kinidhamu ya watoto wao wawapo shule.
Akiongelea suala hilo, mwakilishi wa Mkuu wa Chuo Kikuu huria tawi la Geita Ndg. Samuel Savimbi amesema kuwa mwitikio wa wazazi katika Wilaya ya Geita bado ni mdogo hivyo watendaji wa Kata, mitaa na vijiji waitishe vikao katika maeneo yao ili wazazi hao watambue ni sehemu ya watu muhimu wanaotakiwa kutatua changamoto kwenye shule wanazosoma watoto wao.
Bwana Cosmas Bayaga, Mtendaji wa Kata ya Bombambili ameeleza kuwa chanzo cha tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike ni maadili yasiyofaa waliyonayo watoto kwa sababu asilimia kubwa watoto wa Geita wanaishi na mzazi mmoja ambaye ni mama au bibi ambao mwanafunzi anapopata ujauzito humaliza kesi hizo kifamilia badala ya kuacha sheria ifuate mkondo wake.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita Ndg. Thomas Dimme ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho ametumia fursa hiyo kuwaonya walimu wenye tabia ya kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha na watu binafsi kunaharibu taswira ya utumishi wa Umma na mtumishi wa Umma mwenye tabia hizo anatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita ameziagiza Halmashauri zote katika Wilaya ya Geita kujenga miundombinu ya kuwapokea wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020,pia Watendaji wa kata, mitaa na vijiji wahakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni kwa wakati.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa