Wazazi Waaswa Kuwekeza kwa Watoto
Wazazi na walezi katika Halmashauri ya Mji a Wilaya ya Geita kwa ujumla wametakiwa kutumia raslimali na mali walizonazo kuwaelimisha watoto ili kuwajengea uwezo wangali wadogo katika dhana mbalimbali za uzalishaji mali ili tuweze kuzalisha wataalam wengi wenye tija kwa maslahi ya nchi yetu.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndugu Herman C. Kapufi wakati wa Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika Mtaa wa Nyanguku kata ya Nyanguku, Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameongeza kuwa malezi na makuzi ya watoto ni muhimu katika maendeleo ya nchi lakini wazazi na walezi wengi katika jamii hawatoi fursa ya kutosha kwa watoto ili waweze kutoa mawazo na michango yao katika maamuzi mbalimbali kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla jambo ambalo limewanyima watoto haki yao ya kushiriki.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyanguku Mhe. Elias Ngole amewakumbusha wazazi na walezi kuwapenda, kuwalinda na kuwapeleka watoto shule katika umri unaotakiwa. “ Inasikitisha sana kuona watoto wenye umri wa miaka nane hawajapelekwa shule badala yake wanaagizwa na wazazi kwenda kuchunga mifugo. Kulima na kufanya shughuli mbalimbali za nyumbani.” Aliongeza Mhe. Ngole
Diwani wa Kata ya Nyanguku amewakumbusha wazazi katika kata yake na Kata nyingine za Halmashauri ya Mji wa Geita kuchangia maendeleo ya ujenzi wa madarasa katika Shule za Msingi na Sekondari kwenye maeneo yao na kuwanunulia mahitaji muhimu watoto wao wanaokwenda shule pasipo kusahau jukumu lao la kufuatiliamaendeleo ya kitaaluma na kinidhamu ya watoto wao wanapokuwa shule.
Watoto wa Shule ya Msingi Nyanguku katika risala yao waliyosoma kwa niaba ya watoto wote wa Halmashauri ya Mji wa Geita wameishukuru Serikali kwa kuwapa elimu bure na chanjo mbalimbali zinazowakinga dhidi ya maradhi. Pia wamewaomba wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum kupatiwa haki ya elimu kwa kuandikishwa shule na si kufungiwa majumbani kwani wana haki ya kupata elimu.
Katika Risala ya watoto hao wamewatahadharisha wenzao kujiepusha na mitego ya mali na tamaa inayowavuta kushiriki katika mienendo isiyofaa, Pia wawe wepesi kutoa taarifa katika vyombo mbalimbali vya dola wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Kadhalika wamewasihi wazazi kuwachukulia watoto wote kama wao kwa kuwazaa hivyo wakemee vitendo vyote vilivyo kinyume na maadili vinavyofanywa na watoto kama kuingia katika kumbi za starehe, muziki na video.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 kila mwaka barani Afrika kwa lengo la kutekeleza Azimio la Umoja wa Nchi huru za Afrika katika kuwakumbuka watoto wa Kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouwa kinyama tarehe kama hiyo mwaka 1976 wakati wakidai haki yao ya kutokubaguliwa na haki nyingine za msingi zikiwemo kupewa Elimu, huduma za Afya, Kusikilizwa, Kupendwa na kulindwa. Ujumbe wa Mwaka huu ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tusimwache mtoto nyuma”.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa