Watumishi wa Umma Wilaya ya Geita Wapigwa Msasa
Watumishi wa Umma kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita, Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Taasisi za Umma ndani ya Wilaya ya Geita wamekumbushwa wajibu wao kama watumishi wa Umma kwa kufanya kazi kulingana na sheria, taratibu na weledi wa taaluma zao.
Akizungumza na Watumishi hao Katika ukumbi wa Gedeco, Halmashauri ya Mji Geita Tarehe 29/7/2019 Mratibu wa Utawala wa Utumishi wa Umma Ofisi ya Rais Ikulu kwa niaba ya Katibu Mkuu kiongozi Bw. Francis Mang’ira amesema kuwa Watumishi wa Umma watambue kuwa wao ni daraja kati ya Serikali na Wananchi hivyo kila Mtumishi wa Umma ahakikishe kuwa utekelezaji wa majukumu yake uwezeshe wananchi kufurahia Serikali na Taifa lao na si kuwachonganisha na Serikali.
“Mwananchi anapofika kwenye ofisi yako hakikisha unampa huduma bora na yenye ufanisi pasipo kuchukia hata kama hutafurahishwa na shida iliyomleta kwako, hapo utaweza kukidhi hitaji lake”Aliongeza Bw. Mang’ira. Kadhalika mwananchi yeyote anapokwenda katika ofisi ya Umma Mtumishi wa ofisi husika ahakikishe anampokea kwa heshima, unyenyekevu na lugha yenye staha, pia amsikilize shida yake na hatimaye kumsaidia kumpeleka kwa Mhusika au Idara ambapo atapatiwa huduma anayohitajika.
Kwa upande wake Mratibu Msaidizi wa Utawala wa Utumishi wa Umma Ofisi ya Rais Ikulu Ndugu Abdallah S. Mnongane amewakumbusha wataalam wanaoshughulikia madawati ya malalamiko kufanya kazi zao vizuri, kwa busara na weledi ili matatizo hususan ya wananchi na watumishi yapatiwe ufumbuzi kwa wakati. Pia kuepuka hali iliyojitokeza kwa sasa ambapo wananchi wanapeleka malalamiko yao kwenye ngazi za juu pasipo kufuata utaratibu wa kuanzia kwenye Ofisi zilizoko kwenye maeneo wanayoishi.
Ndg. Mnongane amewakumbusha wakuu wa Idara na Vitengo kuwafuatilia watumishi walio chini yao ili kujiridhisha kma wanafanya kazi, pia vikao vya kila Idara au Vitengo vipangiwe ratiba ya kufanyika angalau mara mbili kwa mwezi ili kuzungumzia mafanikio na changamoto za kila Mtumishi katika Idara husika.
Semina hiyo iliyofanyika kwa Watumishi wa Umma katika Wilaya ya Geita ni sehemu ya majukumu ya Katibu Mkuu Kiongozi ambapo huzungumza na watumishi wa Umma kuzingatia sera,sheria taratibu na miongozo mbalimbali katika Utumishi wa Umma. Pia ni matakwa ya Serikali ya awamu ya tano kwa watumishi wake ambapo kila mtumishi anatakiwa ayatimize.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa