Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya GGML iliyopo mkoani Geita, kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita imetoa mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Geita juu ya kukabiliana na majanga ya moto.
Akitoa mafunzo hayo leo Agosti 12, 2024 katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya mji wa Geita, Kaimu kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Edward Lukuba ameipongeza GGML kwa kuendelea kuiishi dhana yao ya usalama na kueleza kuwa wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha Jamii kuzingatia usalama huku akisisitiza kuwa jukumu la kujikinga na majanga ya moto ni la kila mmoja kwenye jamii.
Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Edward Lukuba akifafanua jambo kwa Watumishi wa Halmashauri.
Bw. Lukuba amesema, anaipongeza GGML kwa kuja na mkakati huo madhubuti wa kutoa mafunzo haya kwa watumishi mbalimbali waliopo katika jengo la Makao Makuu ya Halmashauri. Na anaamini hapo hajatoa elimu kwa watumishi hao tu bali anaamini elimu hiyo itafika hadi majumbani kwa watumishi hao na itasaidia kufanya watu kujikinga na majanga ya moto.
Awali GGML ilitoa mafunzo kwa wanafunzi ambapo jumla ya wanafunzi waliopata elimu shule za sekondari ni 15,091 na walimu 2 kwa halmashauri ya mji na wilaya ya Geita, kama anavyobainisha Kaimu Afisa Elimu Sekondari Bi. Linda Marandu.
Baadhi ya Watumishi wa Halmshauri ya Mji wakiwemo Bw. Justine Mbilinyi na Bi. Valerian Makonda wamesema kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga juu ya kuweza kuchukua tahadhari kuhusu majanga ya moto sio tu hapo ofisini katika jengo la Halmashauri lakini pia hata majumbani ambapo mara nyingi hatari ya moto hutokea na huwa wanashindwa kutoa msaada.
Mtumishi wa Halmashauri ya Mji Geita akifanya Majaribio ya kuzima moto kwa vitendo.
Naye, Bw. Mussa Mbyana akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji ametoa shukrani kwa GGML na Jeshi la zimamoto na uokoaji kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatatusaidia katika kazi zetu za kila siku na amewaomba mafunzo haya yasiishie tu hapa Makao Makuu bali yawafikie na watumishi waliopo nje ya mji na hata jamii kwa ujumla.
Mafunzo yaliyotolewa ni sehemu ya mipango ya GGML katika kuchangia maendeleo ya jamii ambapo wamekuwa wakishirikiana na taasisi nyingine za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama na yenye ustawi kwa Jamii na Taifa kwa ujumla.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa