Watoto wa Kike Watakiwa Kujitambua
Afisa Elimu awali na msingi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Margareth Macha amewausia Watoto wa kike kujitambua thamani zao na umuhimu wao katika jamii siku zote, ili kuepukana na mimba za utotoni, maradhi na vitendo vinavyovunja maadili ya kitanzania.
Bi. Macha ametoa ushauri huo tarehe 11 Oktoba 2023 alipokuwa akihutubia hadhara ya Watoto kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari walioshiriki maadhimisho ya Siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Nyanza Geita mjini.
Afisa Elimu msingi aliongeza kuwa chanzo cha tatizo la watoto wengi kukatishwa masomo ni Watoto wenyewe wa kike kukubali kurubuniwa kwa vishawishi mbalimbali ikiwemo chips, mayai, nyama choma, soda pamoja na vizawadi vidogo.
“Kadhalika baadhi ya Watoto wa kike wameshindwa kuendelea na shule kutokana na changamoto za kifamilia ikiwemo kutengana kwa wazazi kunakopelekea Watoto kukosa malezi na uangalizi wa karibu wa wazazi/walezi. Hivyo wazazi na walezi timizeni wajibu wenu katika malezi ili tuwasaidie Watoto wetu wa kike kutimiza ndoto zao.” Aliongeza Bi. Margareth Macha.
Bi. Macha ametoa wito kwa wenyeviti wa mitaa pamoja na watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya vitongoji kuhakikisha wanawakamata watu wote ambao wamejenga tabia ya kutelekeza familia kwa kisingizio cha ugumu wa Maisha.
Msimamizi wa masuala ya jinsia kutoka mradi wa KAGIS ulioko chini ya Shirika la Plan International Bi. Hildergada Mashauri amesema uwepo wa mradi wa kutetea mtoto wa kike umeisaidia jamii kuondokana na dhana potofu ya kumuona mtoto wa kike kama kiumbe dhaifu asiye na uwezo wa kuwa kiongozi na hivyo kutotoa kipaumbele cha elimu kwa Watoto wa kike.
Siku ya mtoto wa kike duniani huadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka kwa lengo la kuwakumbusha Watoto wa kike juu ya wajibu wao katika jamii na umuhimu wao katika kujitambua na kuepukana na vitendo viovu vitakavyowakwamisha kutofikia ndoto zao. Pia kuendelea kuwasisitiza wazazi juu ya malezi ya Watoto wao. Kwa mwaka 2023 maadhimisho hayo yalibeba kauli mbiu isemayo “Haki zetu ni hatima yetu, Wakati ni sasa.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa