Watoto 78,974 Kukingwa Dhidi Ya Polio Geita Mji
Julma ya watoto 78,974 wenye umri chini ya miaka mitano wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya kuwakinga dhidi ya maakumbikizi ya ugonjwa wa polio wakati wa kampeni lililoanza tarehe 1-4 Septemba 2021
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mratibu wa chanjo Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Mutashubirwa Nestory amesema kuwa zoezi la chanjo litafanyika katika zahanati na vituo vyote vya afya pamoja na kampeni ya nyumba hadi nyumba ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo ametoa rai kwa wananchi wote kutambua umuhimu wa chanjo kwa kuwapeleka watoto wote wenye umri lengwa kuchanjwa na kutowaficha watoto wagonjwa, wenye ulemavu wa aina mbalimbali majumbani kwani haki ya kupatiwa chanjo ni ya kila mtoto pasipo kuangalia mapungufu yake.
Ugonjwa wa Polio unasababishwa na kirusi cha polio ambacho huenezwa kwa kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huo. Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu kwa kutozingatia kanuni za usafi na endapo mtoto mmoja atapata maambukizi, watoto wote watakuwa kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa polio.
Ugonjwa wa Polio hushambulia mifupa ya fahamu na kusababisha kupooza kwa misuli hasa miguu, mikono au vyote kwa pamoja na kwa wakati mwingine misuli ya kifua inayosaidia kupumua na hatimaye kusababisha kifo. Dalili za ugonjwa wa Polio ni pamoja na mgonjwa kuwa na homa kali, mafua, maumivu ya mwili, maumivu ya kichwa na shingo na ulemavu wa ghafla wa viungo.
Ingawaje ugonjwa wa Polio unaweza kuwapata watu wa rika zote, watoto wenye umri chini ya miaka mitano wako kwenye hatari Zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huo. Ugonjwa wa Polio unaweza kuzuiwa kwa kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa huo pamoja na kuzingatia usafi wa mikono, usafi wa mazingira kwa ujumla ikiwemo matumizi sahihi ya choo bora.
Nchini Tanzania chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio hutolewa mara nne kwa mtoto mara anapozaliwa, akifikikisha umri wa majuma sita,kumi na 14 pia wakati wa kampeni maalum zitakapohitajika. Hivyo ni muhimu watoto wapatiwe chanjo wakati wa kampeni za kitaifa hata kama amekamilisha ratiba ya chanjo kwa utaratibu wa kliniki.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa