Watendaji Watakiwa Kusimamia Vyema Mkataba Wa Lishe
Watendaji wa Kata 13 za Halmashauri ya Mji wa Geita wameagizwa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa viashiria vyote vilivyomo katika mkataba wa lishe ili kuleta mabadiliko katika kuboresha hali ya lishe kuanzia ngazi ya kaya hadi jamii nzima pamoja na kuweka utaratibu maalum wa kuadhimisha siku ya lishe kwa kila kata.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Zahara Michuzi hivi karibuni alipokuwa akishuhudia tukio la watendaji wote wa kata kusaini mkataba wa lishe, tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano katika jengo la ofisi ya Halmashauri ya Mji Geita eneo la Magogo Geita mjini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita ameeleza kuwa viashiria vinavyotakiwa kutekelezwa ni pamoja na Watoto kupatiwa chakula mashuleni, wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ipasavyo na kupatiwa madini joto, Watoto kupatiwa vitamin A, Watoto wenye utapiamlo mkali kupatiwa huduma vituoni na utoaji wa fedha ipasavyo kwa ajili ya afua za lishe.
“Watendaji wote hakikisheni mnasimamia vigezo vya upimaji na vipaumbele vya kata kwa kila mwaka ambavyo ni upatikanaji wa taarifa za hali ya lishe kwa Watoto chini ya miaka mitano, kufanya ufuatiliaji wa Watoto walioacha matibabu ya utapiamlo kwa kushirikiana na watoa huduma za afya ngazi ya jamii.” Aliongeza Bi. Zahara Michuzi.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Geita Oscar Obeid amesema kuwa ataendelea kujipanga Zaidi ili kuhakikisha kata zote ndani ya Halmashauri kila kiashiria kinafika asilimia 95 na sio chini ya hapo. Kadhalika kitengo chake kitaendelea kutoa elimu kwa jamii ili wazazi watambue umuhimu wa kuchangia chakula cha Watoto mashuleni ili kukuza kiwango chao cha lishe, kuongeza usikivu na kupunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi.
Utekelezaji wa mkataba wa lishe uliosainiwa utakuwa wa miaka nane kuanzia tarehe mosi Julai 2022 hadi tarehe 30 Juni 2030 kulingana na malengo na shabaha zilizoainishwa katika mikakati ya kitaifa ya muda mfupi, muda wa kati pamoja na muda mrefu ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo yam waka 2025, mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na Sera mbalimbali za nchi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa