Watendaji Wapigwa Msasa Geita Mji
Zaidi ya Watendaji 60 wa Kata, Mitaa na vijiji vya Halmashauri ya Mji wa Geita wamepata fursa ya kupewa mafunzo ya namna ya utendaji bora wa kada zao katika utumishi wa Umma. Mafunzo hayo yametolewa na Afisa Tarafa wa Geita Ndugu Innocent Mabiki, tarehe 26/03/2019 katika ukumbi wa Gedeco Halmashauri ya Mji Geita.
Ndg. Mabiki amewaasa Watendaji hao kuwa mfano bora wa kuigwa katika jumuiya wanazoziongoza kwa kuwa waadilifu, wachapakazi, waaminifu na kufanya kazi kwa weledi wakizingatia kanuni na taratibu za nchi. Kwani kwenda kinyume na hapo watachafua taswira ya Serikali ya awamu ya tano ambayo kwa sasa inafanya mambo makubwa ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Kata na mitaa wanayoisimamia.
“ Pamoja na majukumu yenu ya kila siku, hakikisheni vikao vya kisheria mnavyopanga katika kamati za Kata na vijiji pamoja na mikutano ya hadhara inafanyika na katika mikutano hiyo Agenda ya Ulinzi na Usalama ifanywe kama Agenda ya kudumu ili wananchi wakumbushwe umuhimu wa kulinda usalama wa maeneo yao na nchi kwa ujumla. Pia msipuuzie suala la kuwasomea wananchi taarifa ya Mapato na matumizi wakati wa mikutano ya hadhara kwa lengo la kuwaweka wazi juu ya masuala ya raslimali fedha katika Kata, Mitaa na vijiji vyao.” Aliongeza Ndg. Mabiki.
Akizungumza kwa niaba ya watendaji wenzake, Mwenyekiti wa Watendaji wote ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Kalangalala Bw. Hamad Hussein ametoa shukrani za dhati kwa Katibu Tarafa wa Geita kwa kutambua umuhimu wao katika kukumbushwa juu ya mbinu za utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Kadhalika wametoa ombi kwa Halmashauri na viongozi wa Mkoa kuwapatia mafunzo hayo mara kwa mara ili kuendelea kuwaweka karibu zaidi na taasisi yao na kuboresha utendaji kazi.
Akibainisha changamoto wanazokabiliana nazo Katibu wa Watendaji ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Bombambili Bw. Cosmas Bayaga amesema kuwa watendaji wanahitaji fedha za kuendeshea ofisi zao, usafiri utakaowawezesha kuwatembelea wananchi wao mara kwa mara inapohitajika, uhaba wa majengo ya ofisi za Kata, Mitaa na Vijiji. Pia baadhi ya wananchi bado wanahitaji elimu ya kuchangia shughuli za maendeleo kwani mwitikio uliopo sio wa kuridhisha.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa