Watendaji Wakumbushwa Kutofanya Kazi Kwa Mazoea
Watendaji wa Kata 50 za Halmashauri mbili zinazounda Wilaya ya Geita wamekumbushwa kuachana na desturi ya kufanya kazi kwa mazoea.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Hashim Komba alipokuwa akizungumza na watendaji wa kata 13 za Halmashauri ya Mji Geita pamoja na kata 37 za Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika ukumbi wa EPZA Bombambili Geita mjini hivi karibuni.
Mhe. Hashim Komba ameeleza kuwa hali ya ukusanyaji mapato katika Wilaya ya Geita sio ya kuridhisha sana hivyo watendaji wanapaswa kutambua kuwa wao ni sehemu ya wakusanyaji mapato na kuacha dhana ya kufikiri jukumu la kukusanya mapato ni la Mkurugenzi na timu yake pekee.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amewaagiza watendaji kuwasaidia wakurugenzi wao kuibua vyanzo vyote vya mapato katika maeneo yao na kuhuisha kanzi data za vyanzo vya mapato vilivyopo ili kazi ya kufuatilia mapato yatokanayo na vyanzo hivyo iwe rahisi kwao kama magavana wa maeneo husika na timu za ufuatiliaji mapato kutoka Halmashauri (Task force).
“Pamoja na majukumu yenu ya kila siku jitahidini kutatua kero mnazoletewa na wananchi wenu. Wekeni utaratibu wa dawati la malalamiko linalotembea kuanzia ngazi za vitongoji hadi katani, utaratibu wa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi katika maeneo yenu utasaidia kupunguza msongamano wa wananchi wanaokwenda kwa wingi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kutwa nzima kusubiria foleni ya kusikilizwa na Mkuu wa Wilaya mwenyewe ilhali kero yake ingeweza kutatuliwa na viongozi wa kata”. Aliongeza DC Komba.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Yefred Myenzi amewasihi watendaji wa kata pamoja na watumishi wengine wilayani hapo kutoishi kwa kuogopana bali wawe wepesi kuiga mifano mizuri kwa wanaofanya vizuri zaidi na kuwa tayari kujifunza kila wakati. Pia kila mmoja akae katika nafasi yake kikamilifu kwa kutimiza majukumu yake kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa