Washiriki wa Maonyesho ya Madini Watakiwa Kujiimarisha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewashauri washiriki wa Maonyesho ya pili ya Teknolojia ya Madini kuibuka na mbinu mpya za uchimbaji ambazo zitaimarisha shughuli zao baada ya kumaliza maonyesho hayo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo alipozungumza na hadhara iliyoshiriki uzinduzi rasmi wa Maonyesho ya pili ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika viwanja vya CCM Kalangalala mjini Geita Tarehe 22/9/2019.
Mhe. Kassim Majaliwa amewahimiza wachimbaji wadogo na wakubwa kuitumia kikamilifu taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini Tanzania ili kupata taarifa muhimu na sahihi za kijiolojia pamoja na ushauri wa kitaalam katika utafutaji wa madini. “Kwa kutumia fursa ya uwepo wa Taasisi hiyo kutawaepusha kuwekeza fedha nyingi katika maeneo ambayo hayana madini na hivyo kuepuka kufanya uwekezaji wa kubahatisha ambao hauna tija kwao na Serikali kwa ujumla.” Aliongeza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewaonya wafanyabishara wasiokuwa waaminifu ambao wanajihusisha na utoroshaji wa madini waache mara moja kwani Serikali ipo makini na imejidhatiti vya kutosha kupambana na vitendo hivyo. Pia amewaahidi wachimbaji kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto wanazokutana nazo wachimbaji wadogo ikiwemo matumizi ya teknolojia duni katika uchimbaji na uchenjuaji madini.
Akizungumzia lengo la Maonyesho hayo Mwenyekiti wa maandalizi Mhandisi Chacha Wambura amesema kuwa maonyesho hayo yamelenga kuonyehsa, kukuza, kuimarisha na kuendeleza uchimbaji hususan mdogo wa Dhahabu. Kadhalika kampuni ndogo na kubwa zinazojishughulisha na uchimbaji madini zinapata fursa ya kujitangaza kupitia maonyeho hayo.
Maonyesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini katika Mkoa wa Geita yatahitimishwa tarehe 29/09/2019 ambapo wafanyabiashara tofauti wa Madini na bidhaa nyingine wamejumuika kutangaza shughuli za kiuchumi wanazotekeleza. Kauli mbiu ya mwaka huu ni Madini ni Chachu ya Ukuaji wa Uchumi wa Viwanda “ Tuwekeze kwenye Teknolojia Bora ya Uzalishaji na Tuyatumie Masoko ya Madini.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa