Wanufaika Washauriwa Kuanzisha Viwanda Vidogo
Jumla ya vikundi 33 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao wamenufaika na mikopo isiyo na riba ambayo imetolewa na Halmashauri ya Mji Geita wameshauriwa kutumia fedha hizo kwa kuanzisha viwanda vidogo na kubadilika kutoka kwenye biashara zilizozoeleka na zinafanywa na watu wengi kwenye jamii.
Akiongea wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya hundi za mkopo kwa walengwa katika ukumbi wa Eneo maalum la uwekezaji kiuchumi Bombambili mjini Geita hivi karibuni, Mbunge wa Geita mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu amewasisitiza wanufaika wa mkopo kuanzisha viwanda vidogo ili kuzipa thamani bidhaa zao akitolea mfano wa mafundi cherehani ambao wanaweza kukuza bishara yao na kuwa kiwanda kidogo.
“Wanavikundi mlionufaika na mikopo kutoka Serikalini hakikisheni mnaitumia mikopo hiyo kwa malengo ambayo yamekusudiwa ili kujiletea maendeleo yenu binafsi na jamii kwa ujumla na sio kutumia fedha hizo katika shughuli za sherehe za Noeli na Mwaka mpya.” Aliongeza Mhe. Kanyasu.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewatahadharisha wanufaika wa mikopo hiyo kuacha tabia ya kutorejesha mikopo kwa wakati mpaka wanafikishwa kwenye vyombo vya dola jambo ambalo linasababisha usumbufu usio na tija, bali wanapozalisha mikopo yao ndipo wanawawezesha na wenzao walioomba mikopo kupatiwa kwa wakati muafaka katika awamu nyingine.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa vijana wa Halmashauri ya Mji wa Geita amesema kuwa jumla ya vikundi 33 vikiwemo 18 vya wanawake, 11 vya vijana na 4 vya watu wenye ulemavu vimepatiwa shilingi Milioni 387 kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi. Ndg. Zengo amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya kiasi cha shilingi 906,628,800 ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani kimetengwa kwa ajili ya utoaji mikopo kwa makundi maalum. Pia Halmashauri imeweza kukusanya shilingi 488,694,700 ambazo ni mikopo chechefu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa