Wanawake Watakiwa Kuwa Vinara Kupinga Ukatili
Wanawake waishio katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Geita wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vya kikatili vinavyoendelea kushamiri kila kukicha katika jamii yao wanamoishi ili kujenga Geita yenye upendo, kuthamini utu na heshima ya kila mmoja kulingana na jinsia yake.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Geita Mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu alipomwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita katika kongamano kubwa la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika katika ukumbi wa Gedeco na kujumuisha makundi mbalimbali ya wanawake.
Mhe. Kanyasu ameeleza kuwa awali ya yote wanawake wanatakiwa kupendana kwa kusaidiana na kukwamuana kiuchumi kupitia vikundi vya kijamii vya kuweka na kukopa, kujiunga na vikundi vinavyopatiwa mikopo isiyo na riba kutoka Serikalini na mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha.
Katika kuadhimisha kilele cha siku ya wanawake Duniani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Zahara Michuzi kwa niaba ya wanawake wote wa Halmashauri hiyo amekabidhi vifaa visaidizi kwa wanafunzi Neema Katwale wa Shule ya Sekondari Kisesa, Fatuma Fadhili wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu na Justin Magaka wa Shule ya Sekondari Kasamwa wakiwakilisha wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum katika Mji wa Geita
Kwa upande wa mwanafunzi aliyepatiwa msaada Bi. Neema Katwale ametoa shukrani za dhati kwa watumishi wa Makao makuu ya halmashauri ya Mji Geita kwa kuona umuhimu wake binafsi na wenzao ambao wanahitaji vifaa visaidizi katika Maisha yao ya kila siku.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa tarehe 8/03 kila mwaka kwa lengo la kuenzi mchango unaofanywa na wanawake katika njanya mbalimbali zikiwemo za taasisi ,Serikali na binafsi. Mbegu za siku hii zilipandwa mwaka wa 1908 wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika jiji la New York wakidai kupunguziwa masaa ya kufanya kazi, mishahara bora na haki ya kupiga kura.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa