Wanawake Wahimizwa Kupinga Ukatili
Wanawake katika Halmashauri ya Mji Geita wamehimizwa kupinga vitendo vya kikatili kwa kutoa taarifa sahihi juu ya matukio ya ukatili yanayoendelea katika jamii na kujilinda wao wenyewe, Watoto na kuepuka kufanya ukatili dhidi ya Watoto wanaowalea.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Geita Ndugu Lucy Beda alipomwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita katika maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani yaliyofanyika katika ngazi ya Halmashauri kwenye viwanja vya EPZ Bombambili tarehe 07/03/2024.
Ndugu Lucy Beda ametumia wasaa huo kuwakumbusha wanawake ambao wanajihusisha na vitendo vya kikatili kama kutupa Watoto baada ya kuzaliwa, kuwanyanyasa Watoto wa kufikia na kuwapiga hadi kujeruhi waume zao waache mara moja vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya mtanzania na vitawapelekea kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Wanawake msinyamaze juu ya ukatili wa kijinsia unaoendelea majumbani kwenu ambao mara nyingi unafanywa na jamaa zenu, ndugu zenu na majirani, pazeni sauti ili kupinga vitendo hivyo vitakavyowakwamisha Watoto wenu kukatishwa malengo yao. Kadhalika msiache majukumu yote ya malezi ya Watoto kwa mabinti wasaidizi wa kazi ili kujenga urafiki baina yenu na Watoto.’’ Ameongeza Katibu Tawala Wilaya ya Geita.
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake wote wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Devotha Anthony amesema kuwa wanaiomba Serikali ya awamu ya sita kurejesha utaratibu wa utoaji wa mikopo isiyokuwa na riba ili wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na mtu mmoja mmoja waweze kukuza mitaji yao na kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa lengo la kujikwamua wao binafsi na familia zao.
Afisa Maendeleo ya jamii Bi. Valeria Makonda ameeleza kuwa Halmashauri ya Mji Geita ina kamati za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambazo hushughulikia masuala yote ya ukatili kwa wanawake na watoto kuanzia ngazi za mitaa, vijiji, kata mpaka ngazi ya Halmashauri. Kamati hizo hufanya kazi kwa kushirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na taasisi mbalimbali kama NELICO, VSO, AICT na Plan International zinazojishughulisha na maswala ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kupima na kutathimini kiasi cha utekelezaji wa malengo na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na kusaidia kujenga na kuimarisha mshikamano wa wanawake duniani ni nafasi pia ya kuona juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kumuendeleza mwanamke na kufanya uhamasishaji wa jamii kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na ahadi za Serikali katika kudumisha amani na usawa wa kijinsia.
Maadhimisho ya mwaka 2024 yamebebwa na Kauli Mbiu isemayo ‘ Wekeza kwa Mwanamke Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii ’.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa