Wananchi Watakiwa Kuunga Mkono Juhudi za Serikali
Wananchi katika Mkoa wa Geita wametakiwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa bidii ili dhamira ya dhati ya Serikali inayolenga kuleta maendeleo kwa kila mtanzania iweze kutimizwa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela hivi karibuni alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji Geita kupitia fedha zilizotolewa na Serikali kuu pamoja na fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akizungumza alipokuwa akitembelea mradi wa ujenzi wa Shule maalum ya wasichana katika mkoa wa Geita ambayo inajengwa katika Kata ya Bombambili Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Shigela amewaagiza watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya mtaa ambao wanasimamia ujenzi wa mradi huo kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mradi huo unajengwa katika ubora wa hali ya juu na unakamilika kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Geita pia ameziagiza taasisi za huduma ya umeme, maji, Barabara kuanza kufanya tathimini ya uwekaji wa huduma hizo katika mradi wa Shule maalum ya wasichana ili ifikapo mwezi Januari 2024 wakati wa ufunguzi rasmi wa shule hiyo wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga katika shule hiyo wasipate shida ya kukosekana kwa huduma hizo muhimu.
Mwenyekiti wa mafundi wazawa wanaojenga mradi huo Mhandisi Robert Gabriel ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwaamini na kuwapatia kazi ya ujenzi wa mradi huo ambao umewawezesha kupata fursa ya kupata riziki kwa ajili yao binafsi na familia zao. Pia mafundi hao wamejipanga kujenga majengo yenye ubora wa hali ya juu na kumaliza kazi kwa wakati ili mwezi Januari 2024 shule hiyo iweze kupokea wanafunzi.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata Nyantorotoro katika Kata ya Nyankumbu ambao unajengwa kwa Shilingi 584,280,028 kutoka Serikali kuu, Ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, nyumba pacha ya mganga, kichomea taka, choo cha matundu manne katika Zahanati ya Shinamwendwa Kata ya Nyanguku iliyojengwa kwa Shilingi 231,860,000 za mapato ya ndani, mfuko wa jimbo na nguvu za wananchi pamoja na ujenzi wa Shule maalum ya Sekondari ya wasichana Geita mjini ambayo inajengwa kwa Shilingi Bilioni 3 kutoka Serikali kuu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa