Wananchi Watakiwa Kutobeza Elimu ya Watu Wazima
Wananchi mkoani Geita wameshauriwa kutobeza elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ambayo hutolewa kwa watu waliokosa fursa ya kupata elimu ndani ya mfumo rasmi kwa lengo la kupunguza wimbi kubwa la watu wasiojua kusoma na kuandika pamoja na kujifunza stadi mbalimbali za Maisha.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita wakati wa Maadhimisho ya kilele cha Juma la Elimu ya watu wazima mkoani Geita yaliyofanyika tarehe 18/10/2023 katika viwanja vya Shule ya Msingi Ludete Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Mhe. Magembe amewasisitiza wananchi kuwahamasisha jamii na kusimamia maendeleo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ili kuwatia moyo na kuwawezesha kupata mahitaji yao muhimu katika elimu badala ya kuwacheka na kuwashangaa, kwa kufanya hivyo watawavunja moyo wanafunzi hao kutofikia ndoto zao.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuuletea mkoa wa Geita fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu na kuwawezesha wasichana walioacha masomo kutokana na matatizo mbalimbali ya kifamilia ikiwemo ujauzito kupitia mradi wa SEQUIP, ambapo takwimu zinaonyesha wasichana waliojiunga na masomo kupitia mradi huu katika mkoa wa Geita ni 244.
Afisa Elimu Mkoa wa Geita Mwl. Anthony Mtweve amewaagiza watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya vitongoji hadi kata mkoani Geita kuendelea kuwatafuta wanafunzi ambao wanatakiwa kujiunga na elimu nje ya mfumo rasmi kuhakikisha wanajiunga ili kupunguza wimbi kubwa la watu wasiojua kusoma na kuandika.
Ndugu Mtweve amebainisha changamoto mbalimbali ambazo zinakikabili kitengo cha Elimu ya watu wazima kuwa ni Halmashauri zote mkoani Geita kukosa uwezo wa kibajeti unaotosheleza usimamizi wa elimu ya watu wazima, Uelewa mdogo wa jamii juu ya dhana ya elimu ya watu wazima pamoja na kukosa honoraria kwa walimu wanaowafundisha wanafunzi walio nje ya mfumo rasmi.
Maadhimisho ya Juma la Elimu kwa watu wazima kwa mwaka 2023 yaliongozwa na kauli Mbiu isemayo “ Kukuza Uwezo wa Kusoma na Kuandika kwa Ulimwengu unaobadilika: Kujenga Misingi ya Jamii Endelevu na yenye Amani.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa