Wananchi Watakiwa Kupinga Vitendo Vya Kikatili
Wananchi wa Kata ya Mgusu na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa ujumla wameaswa kuhakikisha kuwa wanapinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea katika maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tarafa wa Geita Ndugu Innocent Mabiki alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita wakati wa Maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizofanyika hivi karibuni katika Kata ya Mgusu.
Ndg. Mabiki ameeleza kuwa kulingana na taarifa zinazotolewa na Idara ya Maendeleo ya jamii katika kata ya Mgusu bado kuna viashiria vinavyoonyesha uwepo wa matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia kwa pande zote mbili na ili kukomesha suala hilo wananchi wanatakiwa kukemea vitendo hivyo na kutoa taarifa kwenye mamlaka za kiserikali pindi vitendo hivyo vinapotendeka.
Afisa Tarafa wa Geita pia ameishauri Idara ya Maendeleo Halmashauri ya mji Geita kujitahidi kutoa elimu / warsha au makongamano ya mara kwa mara kwenye jamii ili wananchi waweze kuelewa athari na kuepuka kutendeana ukatili wa kijinsia.
Mtendaji wa Kata ya Mgusu Victor Bashingwa amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wakati wa utatuzi wa kesi zinazohusisha matendo ya kikatili ni tabia ya upande wa walalamikaji hususan wanawake kukatisha muendelezo wa mashtaka kwa kuomba waume zao wasamehewe kwa ukatili walioufanya kwa wake zao na watoto na kuzifanya kesi hizo kushindwa kufikia hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mratibu wa dawati la Maendeleo ya jinsia Halmashauri ya Mji Geita Bi. Saga Mtaki amesema kuwa ofisi yake hupokea wanawake na watoto ambao huathirika na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikilinganishwa na wanaume. Ukatili huo ni kama vile ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia na ukatili wa kiuchumi. Ambapo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba 2020 wanaume 43, wanawake 215 na watoto 16 wamejitokeza kuleta taarifa na malalamiko.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa