Wananchi Wapongezwa Kwa Kujitoa Kuboresha Miundombinu
Wananchi wa Mtaa wa Nyantorotoro wamepongezwa kwa jitihada zao za dhati katika kuhakikisha wanarekebisha barabara ya Nyantorotoro hadi Mbabane ambayo imeharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Barnabas M. Mapande akiongozana na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Geita wakati wa ziara yao kutembelea maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni, ambapo yeye na timu yake walishiriki katika shughuli ya kupanga mawe kwenye barabara hiyo ili kuruhusu gari nimayosogeza vifaa vya ukarabati kuweza kupita eneo lililoharibika vibaya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita amewaeleza wakazi wa Nyantorotoro kuwa marekebisho ya barabara hiyo yataanza hivi karibuni kwa sababu mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kukarabati ambapo kwa sasa anafanya kazi ya kutengeneza makaravati. Kadhalika amewaahidi kuondokana na kero ya umeme kwa sababu kituo kikubwa cha kupozesha umeme kinajengwa katika eneo la Mpomvu, irani na Mtaa wao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyantorotoro Ndugu Bahati Kaswahili ameiomba Serikali iwasaidie kurekebisha barabara hiyo ambayo ina watumiaji wengi na pia inakwenda kwenye Shule mbili za msingi, hivyo kwa sasa walimu na wanafunzi wanakabiliana na changamoto ya kufika shuleni.
Mhe. Barnabas Mapande ametumia fursa hiyo kutembelea shule ya Sekondari Geita kwa lengo la kuzungumza na wanafunzi, kutambua miradi inayotekelezwa shuleni hapo na kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili. Akiwa shuleni hapo amewataka wanafunzi wajitahidi kusoma kwa bidii ili wafaulu vizuri na kubadilisha matokeo ya shule na kurejesha hisoria ya Geita Sekondari.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa