Wananchi Wakumbushwa Kupima VVU
Wananchi mkoani Geita wameshauriwa kujijengea utamaduni wa kupima Virusi vya UKIMWI mara kwa mara ili kutambua afya zao na kujifunza namna bora ya kuishi na maambukizi ili kujenga afya bora ya mwili na kuzuia maambukizi mapya kutoongezeka.
Kauli hii imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela alipokuwa akihutubia wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Disemba mosi katika viwanja vya CCM Kalangalala Geita mjini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewaeleza wananchi kuwa UKIMWI bado upo na takwimu zinaonesha kuwa maambukizi ya ugonjwa huo katika mkoa wa Geita bado yako juu kwa asilimia 4.7% ambapo wanawake wanaongoza kwa asilimia 60.7%, hivyo kuna umuhimu wa kila mwananchi kutambua afya yake na kuchukua tahadhari.
“Ugonjwa wa UKIMWI unaepukika, mtu anaweza kujikinga asipate maambukizi na wenye maambukizi wafuate kanuni bora za kuishi kwa kula chakula bora chenye vitamin zote na matunda pamoja na kutumia kikamilifu dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI ili watu hao waweze kupata nguvu za kutimiza majukumu yao na hatimaye kutimiza malengo waliyojiwekea.” Aliongeza Mhe. Martine Shigela.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ametumia fursa hiyo kuwaasa wauguzi, madaktari na wahudumu wote wa afya kuwapenda wagonjwa wa UKIMWI na wenye VVU ili waone kwamba kupata ugonjwa huo sio mwisho wa Maisha, kadhalika jamii haipaswi kuwanyanyapaa waathirika wa VVU kwa sababu wao ni watu wa muhimu sana katika jamii.
Akiwasilisha mikakati waliyojipangia kama mkoa, Mratibu wa UKIMWI Mkoa Ndg. Last Lingston amesema kuwa Serikali mkoani Geita kwa kushirikiana na wadau wamejipanga kuendelea kuielimisha jamii juu ya tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU, Kuwahamasisha waajiri kutenga bajeti za mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwenye mipango na kutoa fedha za utekelezaji pamoja na kuwashirikisha viongozi wa kidini ili kuongeza hamasa kwa wanaume kujitokeza kupima VVU na kupunguza unyanyapaa na ukatili wa kijinsia kwa Watoto.
Maadhimisho ya mwaka 2023 yalikuwa na Kauli mbiu isemayo “JAMII IONGOZE KUTOKOMEZA UKIMWI” ikisisitiza kuimarisha ushirikishwaji wa jamii kupitia Asasi za kiraia katika kuongoza mwitikio wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuhakikisha huduma za VVU na UKIMWI zinayafikia makundi mbalimbali kwenye jamii.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa