Wananchi Wakumbushwa Kujenga Desturi ya Mazoezi
Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Geita wametahadharishwa kuwa ukosefu wa mazoezi ya kutosha ya mwili ni moja kati ya mambo hatarishi yanayopelekea watu kuugua magonjwa hivyo wameaswa kujenga desturi ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga kinga mwili na kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza Halmashauri ya Mji Geita Dkt. Annath Mussa Kalokola wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya CCM Kalangalala Geita mjini.
Dkt. Annath Mussa ameeleza kuwa magonjwa kama shinikizo kubwa la damu, kisukari, magonjwa sugu ya kifua,magonjwa ya moyo, kiharusi, kutotengemaa kwa akili, saratani mbalimbali yanaepukika kwa kubadili mtindo wa Maisha, ulaji wa chakula bora na kufanya mazoezi ya mwili.
“Asilimia 33 ya vifo vinavyotokea katika Nchi yetu vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza hivyo tujitahidi kuepukana navyo kwa kupima afya zetu angalau mara moja kwa mwaka. Katika maadhimisho ya mwaka huu wateja 2116 walipimwa shinikizo la juu la damu na watu 58 wamegundulika kuwa na tatizo hilo.” Aliongeza Dkt. Annath Mussa.
Kwa upande wake Afisa michezo wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Juliana Kimaro amewasihi wananchi kuwa na mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara angalau dakika 30 kwa siku na isipungue mara tano kwa wiki pasipo kusubiri maagizo ya viongozi au kampeni za kitaifa kwani mazoezi huzuia uzito au unene uliokithiri na kitambi au kiribatumbo hivyo kujikinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa