Wananchi Wakumbushwa Kujenga Desturi Ya Kupenda Usafi
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Rosemary Senyamule amewaasa wananchi wa wilaya ya Geita na Mkoa mzima kwa ujumla kujenga tabia ya kupenda kufanya usafi katika maeneo yao ya kazi na majumbani pasipo kusubiri kuhamasishwa au kusimamiwa na viongozi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 26/4/2022 aliposhiriki shughuli ya usafi wa mazingira Pamoja na wananchi katika mtaa wa shilabela na Stendi ya mabasi Geita mjini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mhe. Senyamule amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuacha mara moja tabia ya kujisaidia hovyo, kutupa taka sehemu zisizo rasmi bali waanzishe vikundi maalum vitakavyosimamia jukumu la usafi wa mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi kama stendi na kuhakikisha mwananchi atakayekaidi na kushindwa kudumisha usafi kama desturi achukuliwe hatua kwa kutozwa faini kulingana na utaratibu uliowekwa.
“Mkoa wa Geita unaendelea kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa muungano kwa kuunganisha nchi hizi mbili na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia nitumie fursa hii kuwapongeza Marais wote waliopita katika awamu tofauti na walioko madarakani kwa kuendelea kuudumisha na kuuimarisha muungano wetu.” Aliongeza Mhe. Senyamule.
Kadhalika Mkuu wa Mkoa wa Geita amewashukuru wananchi kwa kushiriki vyema katika zoezi la Anwani na Makazi, pia kuwakumbusha kushiriki vyema katika zoezi la Sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwezi Agosti. Mhe. Mkuu wa Mkoa amewasihi wazazi na walezi wote kuwapeleka Watoto wenye umri kuanzia miaka 0 hadi 5 kwenye chanjo ya polio itakayoanza kutolewa tarehe 28/04/2022.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo amewaagiza wananchi wake kufanya usafi kama tabia ambayo wanatakiwa waijenge na sio kusubiri kufanya usafi siku moja kwenye mwezi ambayo ni jumamosi ya mwisho wa mwezi chini ya usimamizi wa wataalam wa usafi na viongozi wao wa mitaa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa