Wananchi Wahimizwa kupanda miti Ili Kutunza Mazingira
Mkuu Wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewahimiza wananchi wilayani Geita kuhakikisha wanapanda miti ya matunda, kivuli, matimba na mbao kwenye kaya zao na mashambani ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuepusha maeneo yao kuwa majangwa.
Mhe. Shimo ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipofanya ziara ya kikazi katika Mtaa wa Nyakato Kata ya Nyanguku kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita na kuzungumza na wakazi wa mtaa huo kwa kuwakumbusha masuala muhimu kwa mustakabali wa maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Akiwa katika mtaa wa Nyakato, Mkuu Wa Wilaya ya Geita amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa vyumba 415 vya madarasa katika Wilaya ya Geita, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ujenzi wa shule maalum ya Sekondari Fulano katika kata ya Shiloleli kupitia maradi wa SEQUIP na mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Viktoria ambao umeshaanza kutekelezwa.
“Nipende kutumia fursa hii kuwapongeza wananchi wa mtaa wa Nyakato kwa kujitoa na kushirikiana na Serikali katika ujenzi na usimamizi wa mradi wa Shule mpya ya sekondari katika mtaa wenu. Nawaagiza kuhakikisha mnakamilisha ujenzi huu mapema ili muhula ujao wanafunzi wanaoenda kupata elimu katika kata Jirani ya Ihanamilo waanze kusomea nyumbani kwao katika madarasa hayo.” Aliongeza Mhe. Shimo
Wazazi wametakiwa kuweka msisitizo katika suala la elimu kwa Watoto wao kwa kukemea utoro wa wanafunzi mashuleni. kadhalika wameshauriwa kuboresha kilimo na kufanya kilimo chenye tija kwa kutumia samadi na mbolea nyinginezo za asili, kilimo chenye tija kitawawezesha kuvuna mazao mengi kwa ajili ya chakula na biashara.
Mhe. Shimo aliwakumbusha viongozi wa mitaa na vijiji kufanya ulinzi shirikishi ili kuwabaini wezi, wauaji na wahalifu wote wanaojitokeza kwenye maeneo yao. Pia wananchi wamekumbushwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23/ 2022 kwa kutoa taaarifa sahihi kwa makarani watakaopita kwenye nyumba zao na kuhakikisha hawawafichi watu wenye ulemavu, wazee sana na wagonjwa wanaoishi kwenye kaya zao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa