Wananchi Waaswa Kutilia Mkazo Zoezi la Chanjo
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela amewaasa wananchi mkoani Geita kuhakikisha wanatilia mkazo chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa kuwaruhusu mabinti walio katika umri lengwa kupata chanjo hiyo muhimu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita hivi karibuni alipokuwa akizindua rasmi zoezi la utoaji chanjo ya HPV kwa ajili ya kuwakinga mabinti wenye umri wa miaka 9 hadi 14 dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, zoezi hilo limezinduliwa kimkoa katika viwanja vya Shule ya msingi Mwatulole Geita mjini.
Mhe. Martine Shigela amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Geita kuwa chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi ni salama na imeshafanyiwa majaribio kadhaa yaliyodhihirisha kuwa haina madhara kwa walengwa waliokusudiwa, kwa kufanya hivyo watakuwa wameunga mkono jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwapatia kinga watoto ambao wanatoka katika hatua ya utoto kwenda kwenye rika la balehe.
Utoaji chanjo ya HPV umeambatana na wiki ya chanjo za kawaida kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano na huduma za lishe ambapo Mkuu wa Mkoa wa Geita aliweza kushiriki katika maandalizi ya uji wenye virutubisho muhimu katika mwili wa binadamu.
Akizungumza wakati wa utoaji wa chanjo hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt Omari Sukari amesema kuwa Mkoa wa Geita umelenga kuwafikia mabinti 276,469 wenye umri kati ya miaka 9 hadi 12 waliopo shule za Msingi, Sekondari na kwenye jamii. Lengo mahsusi ikiwa ni kuzuia na kupambanana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Kauli Mbiu ya Mwaka huu inasema ‘‘Jamii iliyochanjwa ; jamii yenye Afya. ’’
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa