Wananchi Waaswa Kujitoa Katika Ujenzi Wa Miradi
Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Geita wameaswa kujitoa kikamilifu katika utekelezaji wa ujenzi wa Miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa katika kata na mitaa yao kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF).
Ujumbe huo umetolewa tarehe 27/01/2023 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Deogratius J. Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi Wilayani Geita na kukagua ujenzi wa Jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Nyanza na Madarasa mawili, Ofisi moja ya walimu na choo cha matundu sita katika Shule ya Msingi Kivukoni Geita mjini.
Mhe. Ndejembi amewasihi wananchi kutambua upendo ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuuonyesha kwao kwa kuwapatia fedha nyingi ambazo zinatumika katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya TASAF.
“Mhe. Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan anatambua namna ambavyo wananchi mnapambana kuchapa kazi katika maeneo yenu kwa lengo la kujikwamua kiuchumi, ndiyo maana ameendelea kuwaboreshea na kuwajengea miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, miundombinu nk. Hivyo ndugu zangu mjitahidi kuitunza miradi hiyo ili iwanufaishe ninyi na vizazi vyenu, Pia mtambue fedha za TASAF ni za Serikali na sio za mfadhili kama baadhi ya wananchi wanavyofikiri.’’ Aliongeza Mhe. Ndejembi.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita Profesa Godius Kahyarara ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuuwezesha mkoa wa Geita fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya kwa ajili ya kidato cha kwanza 2023, miradi ya afya, maji, umeme, barabara na TASAF ambapo mpaka mwezi Disemba 2022 Halmashauri ya Mji wa Geita imepokea jumla ya Shilingi 799,662,725.82 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Miundombinu chini ya TASAF.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa