Wananchi Geita Wapongezwa Kujitoa Kuchangia Miradi
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ametoa pongezi za dhati kwa wananchi wa kata zote za Halmashauri ya Mji Geita kwa kujitoa kifedha na nguvukazi katika kuchangia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao hususan ujenzi wa vyumba vya madarasa na zahanati.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ametoa pongezi hizo hivi karibuni alipokuwa katika ziara ya kuweka mawe ya msingi kwenye baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Zahanati zilizojengwa na Halmashauri ya Mji kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo pamoja na fedha za wahisani kama Mgodi wa Dhahabu wa Geita.
Mhandisi Robert Gabriel ameongeza kuwa wananchi ambao wamejitoa na wanaendelea kujitoa kwa hali na mali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali wanastahili kupongezwa na kuhamasishwa waendelee na moyo huo kadhalika viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya mtaa na vijiji mnatakiwa kuacha kupiga porojo na kutumia raslimali fedha zilizopo kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kuleta mabadiliko makubwa katika sekta muhimu kama Afya, Elimu na Barabara.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Rashid Muhaya amesema kuwa ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukaranga utasaidia kupunguza idadi ya wanafunzi watoro ambao walikuwa wakibaki nyumbani kutokana na kuchoka kutembea umbali mrefu kwenda shule ya Sekondari Kivukoni umbali wa zaidi ya kilomita tano.
Katika ziara yake ambayo ililenga kuhamasisha jitihada za wananchi katika kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo, Mkuu wa Mkoa wa Geita aliweka mawe ya msingi katika Shule za Sekondari Lukaranga iliyoko katika Kata ya Nyankumbu na Bombambili, Shule ya Msingi Uwanja katika Kata ya Nyankumbu pamoja na Zahanati ya Ikulwa iliyoko Kata ya Ihanamilo zikiwakilisha miradi yote ambayo imejengwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na wananchi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa