Wananchi Geita Wahimizwa Kutunza Miti
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo amewasisitiza wananchi wilayani kwake kuhakikisha wanaitunza miti iliyopandwa na itakayoendelea kupandwa katika maeneo mbalimbali ya makazi, maofisini, shuleni na pembezoni mwa barabara.
Mhe. Shimo ametoa rai hiyo Tarehe 08/12/2022 alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya msingi Mbugani aliposhiriki zoezi la upandaji miti katika shule hiyo ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Juma la Uhuru wa Tanzania Bara hapo tarehe 9 Disemba 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameeleza kuwa kwa kupanda na kutunza miti ni sehemu ya utunzaji mazingira kadhalika zoezi la upandaji miti katika juma la Uhuru ni historia kwa vizazi vijavyo ambapo watakuwa wanakumbuka matukio yaliyofanyika wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru katika Wilaya ya Geita kwa mwaka 2022.
Mhe. Shimo amewaeleza wananchi wa Wilaya ya Geita pamoja na watumishi wa taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi kujenga desturi ya kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao ili kupata faida za miti ikiwa ni pamoja na kuwapatia matunda, kivuli, mbao pia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kurudisha uoto ulioharibiwa.
Kwa upande wake Kaimu Mhifadhi misitu Wilaya ya Geita Ndg. Sandusy C. Nguyale ameeleza kuwa katika Maadhimisho ya juma la miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara jumla ya miti 12,550 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Geita na ameendelea kuwahimiza wananchi na taasisi mbalimbali za Umma na binafsi Kwenda kuchukua miche ya miti katika kitalu cha Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kilichopo eneo la Usindakwe Kata ya Buhalahala Geita mjini na kupanda katika maeneo yao ili kufikia malengo ya kupanda miti 1,500,000 kwa mwaka 2022/2023.
Maadhimisho ya juma la Uhuru wa miaka 61 ya Tanzania Bara yanayoongozwa na kauli isemayo “Miaka 61 ya Uhuru Amani na umoja ni nguzo kwa Maendeleo yetu.” Wilayani Geita yamepambwa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo usafi wa mazingira katika maeneo ya masoko, shuleni na kwenye makazi ya watu, upandaji miti, mashindano ya michezo mbalimbali kwa wanafunzi, midahalo na kutembelea shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalum Mbugani pamoja na wafungwa katika gereza la Geita
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa