Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Hashim Komba amewaasa wananchi wa Wilaya ya Geita kushiriki kuinua uchumi wa Nchi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa wazalendo sambamba na kutafakari kwa kina ndani ya miaka 63 ya Uhuru wa Nchi ya Tanzania walipotoka, walipo sasa na wanapoelekea .
Mhe. Komba ameyazungumza hayo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela kwenye Kongamano la Wadau lililofanyika katika Ukumbi wa Gedeco Halmashauri ya Mji wa Geita wakati wa Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Disemba 2024.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameeleza kuwa waasisi wa Nchi ya Tanzania walitumia uwezo wao na uzalendo wa hali ya juu kuifikisha Nchi ya Tanzania mahali ilipo hususan mafanikio katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, maji, barabara na nyinginezo.
Akizungumza namna maisha yalivyokuwa kipindi Nchi ya Tanzania inapata uhuru, Mzee Samwel Majura ambaye ana umri wa miaka 75 ametoa rai kwa vijana wa sasa kuacha tabia ya kuibeza Serikali kuwa haijafanya lolote wakati katika kipindi cha nyuma wananchi walitembea umbali wa Zaidi ya kilomita 20 kufuata huduma za afya katika Hospitali moja tu iliyokuwa Geita mjini hali iliyopelekea baadhi ya kina mama kujifungulia njiani lakini ndani ya miaka 63 ya Uhuru Serikali imejenga zahanati kila kijiji na vituo vya afya vya kutosha.
Kwa upande wake Mzee James Zomola mwenyeji wa Wilaya ya Geita ambaye alianza elimu yake katika darasa maarufu kipindi hicho “Bush School” ameeleza kuwa wakati Nchi inapata uhuru kutoka kwa wakoloni shule zilikuwa chache sana na hakukuwa na walimu wa kutosha hali iliyosababisha wanafunzi wengi kushindwa kuendelea na masomo, kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari ilikuwa ni bahati sana lakini sasa hivi Serikali imejenga shule nzuri za sekondari kila kata na zenye walimu wa kutosha.
“ Mimi binafsi naweza kutoa ushuhuda wa Sekta ya maji kwa namna ambavyo ndani ya kipindi cha miaka 63 ya Uhuru imeboreshwa kwa kiwango kikubwa sana, wananchi wanapata huduma za maji majumbani kwao au jirani kabisa na maeneo wanayoishi tofauti na miaka ya nyuma ambapo maji yaliyotumika yalitokana na chemichemi, mito na maziwa. Nakumbuka kwa wakazi wa Kata ya Kasamwa ambao chanzo chetu cha maji ilikuwa ni chemichemi wakati wa kiangazi maji yalikuwa yanakauka na kulazimu watu wenye baiskeli tu kufuata maji Geita mjini katika kisima cha asili Lwenge.” Aliongeza Mzee James Zomola.
Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Mkoa wa Geita yaliyobebwa na kauli mbiu isemayo “Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara: Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi wa maendeleo yetu.” Kadhalika wananchi waliohudhuria katika Kongamano la Uhuru walipata kufahamu Historia ya harakati za kupata Uhuru wa Tanzania na mchango wa viongozi wa Taifa katika Maendeleo ya kiuchumi, Tanzania na harakati za mapinduzi ya kiuchumi katika sekta za elimu, afya, maendeleo ya jamii, kilimo, miundombinu, nishati, biashara, mawasiliano na ujenzi kupitia mada zilizowasilishwa na wataalam wa kada mbalimbali.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa