Wanafunzi Wajipatia Vifaa vya Usafi Kutoka Plan International
Jumla ya Shule 77 za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Geita na Wilaya ya Geita wamepatiwa vifaa vya usafi ambavyo ni sabuni,taulo za kike, vifaa vya kunawia mikono,vifaa vya shule kama madaftari na kalamu kutoka Shirika la Plan International Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika Tarehe 10/8/2020 katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyanza Geita mjini Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amelishukuru shirika la Plan kwa kutoa vifaa vya usafi mashuleni ambavyo vitawasaidia wanafunzi kujikinga na maradhi mbalimbali kama magonjwa ya kuhara, kipindupindu, trakoma na magonjwa ya macho na ngozi.
Mhandisi Robert Gabriel ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Geita itaendelea kulienzi shirika la Plan kwa mazuri wanayoyatenda na kuyataka mashirika mengine kuiga mfano wa Shirika la Plan. Pia amelipongeza shirika hilo kwa kutoa elimu juu ya namna bora ya unawaji mikono kwa makundi mbalimbali kama watu wenye ulemavu, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na walimu 680 kutoka shule za Msingi na Sekondari katika Wilaya ya Geita.
“Nina Imani kuwa wananchi wa Geita kwa sehemu kubwa wamenuafaika kwa elimu iliyotolewa kwa makundi mbalimbali ambapo walifundishwa namna ya kunawa mikono kipindi nchi yetu ilipokuwa inajikinga na ugonjwa wa Corona. Pia napenda nitoe wito kwa wanafunzi wote mtakaonufaika na vifaa hivi vya usafi kusoma kwa bidi ili muweze kufanikiwa kwenye maisha yenu ya baadaye.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Mkoa wa Geita Ndg. Adolf Kaindoa amesema kuwa Shirika la Plan International limeona ni vyema kutoa vifaa vya usafi hasa sabuni za maji katika juhudi zake za kuhakikisha watoto wanalindwa na magonjwa ya mlipuko ambapo kila shule itapatiwa galoni 10 za sabuni ya maji.Kadhalika Shirika limetoa 62(Tippy-Taps) vya kunawia mikono kwa watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Geita, vifaa ambavyo vitapelekwa kwenye vituo vya afya ili kulinda afya zao dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu.
Ndugu Kaindoa ameahidi kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuweka mikakati zaidi ya kuhakikisha haki za msingi za watoto, changamoto mbalimbali zinazowakabili zinatafutiwa ufumbuzi. Pia kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa watoto vinatokomezwa katika Mkoa wa Geita.
Akiongea kwa niaba ya walimu wa shule zilizonufaika Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu Mwl. Georgia Mugashe amelishukuru Shirika la Plan kwa huduma kubwa na ya mfano waliyoitoa hususani ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi kwa sababu kuna baadhi ya mabinti wanapata changamoto kubwa shuleni wanapokuwa katika kipindi cha hedhi kwa kukosa vifaa vya uhakika vya kujisitiri.
Vifaa vya kunawia mikono,Taulo za wanafunzi wa kike, sabuni, madaftari na kalamu kwa shule 77 za msingi na sekondari pamoja na vituo vya afya katika Halmashauri mbili za Wilaya ya Geita vilivyotolewa na Shirika la Plan International Tanzania vimegharimu jumla ya Shilingi 63,960,000/= za kitanzania.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa