Walimu Watakiwa Kuimarisha Vipindi Vya Dini Mashuleni
Walimu wa Shule zote za msingi na sekondari nchini wametakiwa kuimarisha ufundishaji wa somo la dini kwa wanafunzi ili Watoto hao wakue kiimani na kuwa na hofu ya Mungu itakayowawezesha kuishi mazingira yoyote katika misingi ya maadili mema.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa ana Serikali za Mitaa Mhe. David Silinde wakati wa ziara yake alipotembelea utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya elimu na barabara ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni.
Mhe. Silinde alitoa wazo hilo baada ya kukagua miundombinu ya maabara, darasa na bweni moja la wanafunzi ambayo imeharibiwa kwa kuchomwa moto katika Shule ya Sekondari Geita kwa nyakati tatu tofauti na kutamka kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wanafunzi wote watakaobainika kushiriki katika matukio yote maovu na waliohusika katika uharibifu wa miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.
“Wazazi ndio kitovu kikuu cha malezi ya Watoto, tafadhali timizeni wajibu wenu katika kuhakikisha mnawalea Watoto wenu katika misingi inayokubalika ili kujenga taifa lenye maadili, Kadhalika walimu mnatakiwa kudhibiti nidhamu ya wanafunzi wenu wanapokuwa shule maana huo ni wajibu wenu kama walezi wa hawa wanafunzi.” Aliogeza Naibu Waziri Tamisemi.
Akikagua ujenzi wa madarasa ya kisasa katika Shule ya Msingi Ukombozi Mhe. Silinde ametoa pongezi kwa uongozi wa Shule hiyo na kata nzima ya Nyankumbu kwa ubunifu wa kutumia milioni 64 waliyopewa na Serikali kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) kujenga madarasa 5 na mashimo 13 ya vyoo badala ya madarasa 3 na mashimo 4 ya vyoo.
Naibu Waziri Tamisemi amempongeza Diwani wa Kata ya Buhalahala Mhe. Dotto Zanzui Ludeha kwa moyo wa majitoleo ya ardhi aliyoitoa bure kwa wananchi wa kata yake ambapo shule mpya ya msingi inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 250 za huduma za kampuni kwa jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita. Mhe. Silinde aliwashukuru kampuni ya GGM kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Miradi mingine iliyotembelewa na Naibu Waziri wa Tamisemi wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Mji Geita ni Pamoja na ujenzi wa barabara ya Mwanza junction hadi Sirro Barracks kwa kiwango cha lami, ujenzi wa barabara ya Upendo Dispesary- American chips kwa kiwango cha lami nyepesi, Maktaba ya wanafunzi na mabweni mawili mapya katika Shule ya Sekondari Geita Pamoja na ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Mwatulole.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa