Walimu 668 Geita Mji Wanufaika na Vishikwambi
Jumla ya wataalam 668 kutoka Idara za Elimu msingi, Sekondari, Waratibu Elimu Kata pamoja na walimu wa shule zote za umma za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Mji Geita wamegawiwa vishikwambi (Tablets) ambazo zilinunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na Makazi mwaka 2022.
Akikabidhi vishikwambi hivyo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Tarehe 18/1/2023 wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi walimu iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri mtaa wa Magogo, Mthibiti ubora wa shule Halmashauri ya Mji Geita Bi. Violet Kiiza ameeleza kuwa baada ya zoezi la Sensa ya watu na Makazi kukamilika Serikali iliazimia kuvigawa kwa sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi za kila siku na kuleta ufanisi kwenye taaluma.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndugu Egidy Teulas amewaasa walimu waliopewa vishikwambi hivyo kuvitumia kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za taaluma shuleni, utunzaji wa takwimu sahihi za idadi ya wanafunzi, miundombinu ya shule pamoja na kuperuzi taarifa mbalimbali zitakazowezesha kuboresha taaluma ya wanafunzi.
“ Sitarajii mwalimu hata mmoja ambaye amepatiwa kishikwambi leo baada ya siku kadhaa nipate taarifa anakitumia katika matukio mbalimbali ya kihalifu yanayoendelea kwenye jamii au Kwenda nacho sehemu za starehe na kuvitelekeza huko, bali mnatakiwa mhakikishe mnatunza mali za Serikali ili viweze kudumu na kuwanufaisha walengwa.” Aliongeza Ndg. Egidy Teulas.
Wakitoa neno la shukrani kwa niaba ya walimu wote Bw. Brighton Samuel Mratibu Elimu kata ya Kasamwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kivukoni Ndg. Ndatu Said Maduka wameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwachagua walimu kupatiwa vishikwambi hivyo miongoni mwa watumishi wote wa umma katika kada mbalimbali.
Walimu hao wameahidi kutovitumia vishikwambi hivyo katika matukio ambayo ni kinyume cha sheria na taratibu za utumishi wa umma bali vitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa ikiwemo kupata taarifa muhimu za kitaaluma kwa haraka na manufaa yake yataonekana baada ya kipindi kifupi kwani kazi zao zitaboreshwa Zaidi kupitia vitendea kazi hivyo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa