Walengwa 48 Wanufaika na Mbuzi 102 Kutoka TASAF
Jumla ya walengwa 48 ambao wamejiunga katika vikundi vinne vya wanufaika wa Mradi wa kuongeza kipato chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini(TASAF) katika kata ya Kanyala wamepatiwa mbuzi 102 wenye thamani ya Shilingi Milioni 22.33
Akikabidhi mbuzi hao kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Afisa Maendeleo ya jamii Bi. Saga Mtaki amewaasa wanufaika kuhakikisha wanawatunza mbuzi hao kwa kuwajengea mabanda bora, kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha, wanapatiwa chanjo na matibabu yanapohitajika pamoja na kuhakikisha wanachungwa katika mazingira salama ili waweze kufaidika kupitia mbuzi hao.
Diwani wa Kata ya Kanyala Mheshimiwa Enock Mapande amewaeleza wananchi wa kata yake watambue namna Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyowapenda na kuwathamini wananchi wake hivyo wananchi wanatakiwa watunze mali waliyopewa ili wazaliane na kuwaondoa kwenye Maisha ya chini na kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wa mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Amani Madenge ameeleza kuwa mbuzi waliotolewa ni zoezi endelevu la mradi wa kuongeza kipato kwa jamii ambao unalenga kuongeza idadi ya mbuzi kwa walengwa baada ya miezi kadhaa.
Mratibu wa TASAF ameongeza kuwa mradi huo unatarajia kuwapatia walengwa mbuzi 238, mbuzi jike 190 na dume 48 ambapo mbuzi watagawiwa kwa vikundi vilivyopo katika Kata ya Kanyala na Kata ya Bung’wangoko. Kwa awamu ya kwanza vikundi vilivyonufaika ni pamoja na ushirikiano majengo, Upendo butendeni, Mwanamke jitambue na kikundi cha Amani Chanama.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa