Wakurugenzi Waagizwa kutenga Bajeti za Madampo
Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Geita wameagizwa kuandaa bajeti za ujenzi wa madampo ya kisasa ili usafi unapofanyika taka ziweze kuhifadhiwa na kuchakatwa bila kuchafua mazingira.
Agizo hilo limetolewa na Kaimu katibu Tawala mkoa wa Geita Ndg. Herman Matemu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Geita akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani mwaka 2022 yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya shule ya sekondari ya Wasichana Nyankumbu Geita mjini hivi karibuni.
Ndg. Matemu amesema kuwa Halmashauri zinapoandaa bajeti zao wahakikishe kwamba zinakuwa na bajeti hiyo ili madampo ya kisasa yaweze kujengwa katika kila Halmashauri. Pia amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuanzia ngazi ya familia kujitafakari ni kwa kiasi gani maamuzi anayoyafanya yanaweza kutunza mazingira na kwa ngazi ya taasisi ni kwa kiasi gani waajiri na wenye mamlaka wanatambua umuhimu wa mazingira na kuhamasisha upandaji miti.
Katika taarifa ya utekelezaji wa uhifadhi wa mazingira iliyosomwa na kaimu katibu tawala mkoa Geita Charles Chacha, imebainika kwamba hali ya mazingira katika machimbo hutofautiana ambapo wachimbaji wakubwa na wakati ni salama kwa shughuli za hifadhi za mazingira huku wachimbaji wadogo ndiyo wenye changamoto katika uhifadhi wa mazingira.
Taarifa hiyo imebainisha kwamba mkoa wa Geita una misitu hekta laki mbili mia tano hamsini na nane nukta tatu (200,558.3) kati ya maeneo hayo sita yanamilikiwa na wakala wa misitu Tanzania- TFS, maeneo mengine sita yanamilikiwa na mamlaka za Serikali za mitaa.
“Pamoja na kuwa na misitu ya asili mkoa wa Geita umepanda miti milioni tatu, mia nane ishirini na tano ,mia tatu kumi na tatu kwa mwaka wa 2021/2022” alisoma Charles chacha.
Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kwamba Malengo ya upandaji miti ilikuwa ni kufikia milioni tisa lakini, miti iliyopandwa ni milioni tatu, mia nane ishirini na tano ,mia tatu kumi na tatu na miti iliyopona ni milioni tatu themanini elfu mia saba hamsini na tatu huku miti hiyo iliyopandwa ni sawa na asilimia 42.5% .
Charles Chacha amesema changamoto kubwa iliyokwamisha kufikia malengo ni upungufu wa miche ya miti, hivyo serikali imeweka mikakati ya kuyafikia malengo hayo kwa kutumia taasisi zake 66 za elimu na mpaka sasa miche milioni mbili imeshapatikana.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa