Wakulima Washauriwa Kulima Pamba Kibiashara
Wakulima wilayani Geita wameshauriwa kubadilisha mfumo wa kilimo cha pamba ili kuinua kilimo hicho na kufanya kiwe kilimo cha biashara kama ilivyo kwa mazao mengine.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg. Herman Kapufi wakati wa Kikao na Maafisa Ugani, Watendaji wa Kata na Wataalam wa Kilimo kutoka kata zote za Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya, kilichofanyika Tarehe 23/8/2017 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amewaagiza Maafisa Ugani na Wataalamu wa Kilimo kutoka Halmashauri hizo kuhakikisha kuwa katika msimu wa kilimo unaotarajia kuanza kilimo cha mkataba kitiliwe mkazo ili kupata matokeo makubwa ya zao la pamba na kuongeza mapato ya Halmashauri na pato la Taifa kwa ujumla.
Amefafanua kuwa baadhi ya mikakati ambayo itafanikisha kilimo cha pamba chenye tija ni pamoja na Kutumia kilimo cha mkataba , Maafisa ugani wawezeshwe kupata usafiri utakaowasaidia kusafiri umbali mrefu kufuatilia mashamba ya pamba, Wakulima wahamasishwe kutokwepa kulima pamba katika maeneo yote na kuainisha mahitaji muhimu katika kilimo cha pamba.
Kwa upande wake Mshauri wa mfumo wa kilimo cha Mkataba kutoka Taasisi ya Gasp Afica Ndg. Joshua Mirumbe amesema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa uzalishaji wa zao la pamba umeshuka kutoka kilo milioni 40 miaka 7 iliyopita hadi kilo milioni 12 kwa sasa katika Mkoa wa Geita, hali hii imepelekea viwanda vya kuchambua pamba vilivyoko nchini kukosa malighafi ya kufanyia kazi.
Ndg. Mirumbe amaeongeza kuwa Maafisa ugani wanatakiwa waunge mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha mfumo wa kilimo cha mkataba kwa sababu wakijipanga vyema ni mfumo ambao utaleta matokeo chanya ya uzalishaji. Pia unaipa nguvu Serikali kusimamia vyema kwa sababu Kampuni itakayohitaji kufanya kazi na wakulima kutambulisha utaratibu wa huduma zake na kushirikiana na Halmashauri husika katika utekelezaji.
“Watendaji wa kata zote mnatakiwa kuwa wasimamizi wakuu kwa kujua shughuli zote jinsi zitakavyofanyika katika maeneo yenu pindi utekelezaji utakapoanza. Pia msihusishe na kilimo cha pamba kilichokuwa kikisimamiwa na Umoja wa Wachambuzi wa Pamba( UMWAPA) ambacho hakikufanikiwa kwa sababu sekta binafsi ziliruhusiwa kufanya kazi moja kwa moja na mkulima pasipo usimamizi wa Serikali.” Aliongeza Ndg. Mirumbe.
Akizungumza kwa niaba ya wataalamu wa kilimo Ndg. Daniel Kulunguja ametoa ushauri wa kuwa na kampuni Zaidi ya moja itakayotumika kugawa pembejeo za kilimo cha zao la Pamba ili kuleta ushindani wa kibiashara na ufanisi wa Kilimo cha mkataba.
Mfumo wa Kilimo cha Mkataba kwa zao la pamba ni utaratibu uliowekwa na Serikali ambapo Kampuni za Uchambuzi wa Pamba hutoa kwa mkopo mbegu, dawa za kunyunyiza, mabomba ya kunyunyizia dawa kwa wakulima wa zao la pamba katika maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania ambako zao la pamba linalimwa na marejesho ya mkopo huo hufanyika baada ya wakulima hao kuvuna pamba zao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa