Wakulima Wahimizwa Kulima Kwa Tija
Wakulima katika Wilaya ya Geita wamehamasishwa kulima kisasa na kitaalam Zaidi ili kuboresha Maisha yao binafsi, jamii nzima na kuongeza pato la Taifa litokanalo na kilimo.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Tarafa za Kasamwa na Geita kwa lengo la kuzungumza na wakulima hususan wa zao la pamba kabla ya kuanza msimu wa kilimo hivi karibuni
Mhe. Shimo ameongeza kuwa ni dhahiri kila mtanzania anatambua mchango wa maendeleo ya kilimo katika nchi hii, uzalishaji wa mazao bado si wa kuridhisha sana hivyo ni jukumu lake kama kiongozi kushauri na kuwakumbusha wakulima wa zao la pamba na mazao mengine kuzalisha kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuwa na kilimo chenye tija.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amewataka mawakala wa pembejeo za kilimo kuwasilisha mahitaji yote kwa wakulima kabla ya msimu wa kilimo kuanza na kuwatahadharisha wakulima kuepuka tabia za uvivu, kesi zisizo na msingi, kuzurula hovyo katika msimu wa kilimo badala yake wajitahidi kuendana na ratiba za kilimo
“Natoa agizo kwa vyama vote vya msingi vya kilimo na ushirika (AMCOS) kulima shamba la ekari tano kwa kila chama katika msimu unaoanza karibuni Kadhalika maafisa ugani katika kata zote wahakikishe hawakai maofisini bali wanatoka kwenda mashambani kuwasaidia wakulima na wao pia wanatakiwa kuanzisha mashamba darasa ya mfano katika kila kata ili wakulima wajifunze kwa vitendo”. Aliongeza Mhe. Shimo
Kwa upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Afisa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji Bw. Leonard Chacha amewaahidi wakulima kuwa yeye na maafisa ugani wake watashirikiana kuhakikisha changamoto zote zitakazojitokeza kwenye mashamba yao zinapatiwa ufumbuzi kwa muda muafaka.
Mkaguzi wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba Tanzania Pamoja na wataalam wa ugani wa Halmashauri ya Mji Geita wametoa elimu ya vitendo juu ya kanuni kumi za kilimo bora cha pamba baadhi ni Pamoja na kutumia mbolea za samadi na virutubisho vingine, kupanda pamba mapema, kupanda kwa mistari na nafasi maalum, kupanda idadi halisi ya mbegu katika kila shimo, kupalilia kwa wakati , kunyunyiza madawa kuzuia wadudu waharibifu na kuvuna pamba mapema.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa