Wajumbe ALAT Wapongeza Miradi ya Mji Geita
Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( ALAT) Mkoa wa Geita wamepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Mji wa Geita katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo yenye kiwango cha hali ya juu.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara waliyoifanya wajumbe hao hivi karibuni katika Halmashauri ya Mji Geita ambapo walitembelea miradi ya ujenzi wa Soko kuu Geita mjini, Barabara ya lami Madini- Bomani- KKKT, Kikundi cha vijana kinachojishughulisha na ufugaji kuku katika mtaa wa Katoma na Ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Bombambili.
Akizungumza walipotembelea ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Bombambili, Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Geita Mhe. Elisha Lupuga amemsifu Diwani wa Kata ya Bombambili pamoja na watumishi wake pamoja na Menejimenti nzima ya Hlmashauri ya Mji wa Geita kwa ujenzi huo wa Ofisi nadhifu na kuahidi kuchangia Shilingi 2,000,000/= kutoka mfuko wa ALAT kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Afisa Tawala msaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Bi. Sania Mwangakala pamoja na pongezi alizozitoa kwa Halmashauri ya Mji wa Geita amewataka wajumbe kutoka kwenye Halmashauri nyingine ndani ya Mkoa wa Geita waige mfano kwa kujenga ofisi za mitaa, vijiji na Kata katika maeneo yao ili watumishi walioko katika maeneo hayo wapate mazingira rafiki ya kufanyia kazi.
Akizungumza katika mtaa wa Katoma walipotembelea kikundi cha Penye nia ambacho kinajishughulisha na ufugaji kuku wa kisasa ambacho kimekopeshwa Shilingi 5,000,000/=kutoka katika asilimia tano ya Mapato ya ndani ya Halmashauri na chenye wanachama watano, Mhe. Safari Mayala, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe amewashauri wanachama kutafuta eneo kubwa kwa ajili ya ufugaji kuku utakaowapatia faida zaidi kuliko eneo walilonalo hivi sasa.
Timu ya Wajumbe wa ALAT Mkoa wa Geita wamefanya ziara hiyo katika Halmashauri ya Mji wa Geita ikiwa ni sehemu ya kikao chao cha robo ya tatu ambapo hufanya vikao vyao kila robo ya Mwaka wa fedha katika Halmashauri za Mkoa wa Geita kulingana na ratiba ya mzunguko waliopanga.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa