Wajasiriamali Watakiwa kuwa Waaminifu
Wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na biashara mbalimbali katika Wilaya ya Geita wameagizwa kuwa wakweli na waaminifu katika utoaji wa taarifa zao binafsi na kuwasilisha vielelezo vya muhimu vinavyohitajika katika biashara zao wakati wa zoezi la ugawaji vitambulisho vya wajasiriamali wadogo linaloendelea katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Geita.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Josephat Maganga alipokuwa akizindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya bei nafuu katika Wilaya ya Geita, uzinduzi uliofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Gedeco Halmashauri ya Mji wa Geita.
Mheshimiwa Maganga ametoa rai hiyo na kusisitiza kuwa wafanyabiashara wakubwa ambao biashara zao zimekwishatambliwa na TRA wasitumie mwanya huo kwa kuwatumia wajasiriamali wadogo kuwaandikishia majina kwa lengo la kukwepa kuchangia mapato halali ya Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Geita pia amewaagiza wajumbe wa kamati ya usimamizi wa zoezi hilo ambao ni watumishi kuanzia ngazi ya vitongoji hadi Ofisi za Halmashauri kuifanya kazi hiyo kwa weledi na uaminifu mkubwa wakitamua kuwa kazi hiyo imeasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo haki inapaswa kutendeka.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Geita Ndg. James Jilala ameainisha sifa za watakaopatiwa vitambulisho hivyo kuwa ni pamoja na biashara zao kutosajiliwa na Mamlaka ya mapato, mauzo ghafi ya biashara zao yasizidi shilingi milioni nne pia watatakiwa kulipia shilingi elfu ishirini kwa mwaka.
Ndg. Jilala ameongeza kuwa wajasiriamali hao wanatakiwa watambue kwamba nia ya Serikali katika zoezi hilo ni kuwainua ili wakue na kuwa na biashara kubwa zitakazowawezesha kuchangia katika pato la Taifa mara baada ya wao kukua zaidi kibiashara.
Jumla ya wajasiriamali 3316 wametambuliwa katika kata 13 za Halmashauri ya Mji Geita na wote watapatiwa vitambulisho katika zoezi linaloendelea katika maeneo mbalimbali ndani ya Mji wa Geita na nchi nzima kwa ujumla.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa