Wahandisi Wahimizwa Kutimiza Wajibu
Wahandisi katika Halmashauri ya Mji Geita wamekumbushwa kutimiza wajibu wao kwa kusimamia ujenzi wa miradi kikamilifu ili kuwa na majengo imara na yenye ubora ambayo yatawanufaisha wananchi katika maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Geita walipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2023.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Ndugu Barnabas Mapande ametoa pongezi za dhati kwa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa Halmashauri ya Mji Geita kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ndg. Barnabas Mapande amewapongeza wananchi wa mtaa wa Mwilima Kata ya Kanyala na Mbunge wa jimbo la Geita mjini kwa kuanzisha mradi wa Zahanati ili kuondoa kero ya wagonjwa hususan wanawake wajawazito na Watoto wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika Kituo cha Afya Kasamwa.
“Mwishoni mwa mwaka 2025 mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika miji 28 Tanzania utakamilika na kuifanya Geita kujivunia mafanikio ya kupata maji mengi ikiwa ni mojawapo ya jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya uhakika ya maji safi na salama.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe ameahidi kushirikiana na Mamlaka ya Maji safi Mjini Geita kusimamia mradi huo na kuhakikisha unakamilika ndani ya muda uliopangwa ili wananchi wa Wilaya ya Geita waweze kuondokana na kero ya upungufu wa maji unaopelekea maji kutoka kwa zamu.
Wakiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Geita wajumbe wa Kamati ya Siasa wamempongeza Diwani wa Kata ya Bombambili inapojengwa shule hiyo Mhe. Leonard Bugomola kwa namna anavyojitoa kutatua changamoto mbalimbali na kuhakikisha miradi katika Kata yake inatekelezwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Geita Bi. Paulina Majogoro amesema kuwa Shule ya Sekondari ya wasichana Geita itawakomboa Watoto wa kike ambao Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia kuwawezesha kutimiza ndoto zao kupitia fursa ya elimu bila malipo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara kata ya Kasamwa Bw. Faustine Kitula ameeleza kuwa ujenzi wa Barabara ya lami kwa kiwango cha lami nyepesi kilomita 0.5 Kasamwa senta utakapokamilika wataepukana na vumbi katika maduka na biashara zao zilizoko pembezoni mwa Barabara hiyo.
Miradi iliyotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Geita ni ujenzi wa Shule ya SekondariNyantoroto, ujenzi wa Shule ya Sekondari ya kitaifa ya wasichana Geita, mradi mkubwa wa maji, kutembelea kikundi cha vijana wanaojishughulisha na uuzaji wa viatu vua mitumba ambacho kimenufaika na mkopo uliotolewa na Halmashauri, ujenzi wa Zahanati ya Mwilima pamoja na ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami nyepesi Kasamwa senta.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa